"Nandy kupata mimba kabla ya ndoa ni ishara ya malezi mabaya, tamaa ya ndoa" - Mwijaku

Nandy na Billnass wanatarajia kufanya harusi hivi karibuni.

Muhtasari

• "Alafu bora ungefanya siri sio unatangaza kabisa hadharani na unamshukuru mungu kweli?" - Mwijaku amwambia Nandy.

Wachu8mba Billnass na Nandy, Mwijaku
Wachu8mba Billnass na Nandy, Mwijaku
Image: Instagram

Mtangazaji wa Clouds FM nchini Tanzania, Mwijaku baada ya kuteuliwa kama mmoja kwenye kamati ya kushughulikia harusi ya Nandy na Billnass, kamati ambayo inaongozwa na muigizaji Steve Nyerere, sasa anakosoa kitendo cha Nandy kuwa mjamzito.

Hii ni baada ya Nandy kuweka bayana kupitia picha alizozipakia kwenye ukurasa wake wa Instagram kuonesha kwamba ana ujauzito mkubwa.

“Swali je kwa nini @officialnandy abebe mimba kabla ya ndoa? Je malezi ya wazazi yalikuwa na changamoto? Au tamaa ya kulazimisha ndoa ujanani?” aliuliza Mwijaku.

Kulingana na Mwijaku, Nandy hangefaa kupata mimba kabla ya harusi yao ambayo ishatangazwa na Nyerere. Mtangazaji huyo mwenye utata amekosoa kitendo cha Nandy kupata ujauzito nje ya ndoa, licha ya kwamba walivishana pete za uchumba lakini bado hawajakuwa wanandoa rasmi kupitia harusi.

Mwijaku anahoji kwamba wawili hao hawafai kupongezwa kwa kuweka wazi suala la ujauzito kwani pongezi hizo zinafaa kuelekezwa kwa watu walioko katika ndoa pekee.

“Alafu kila mtu anampa pongezi @officialnandy na @billnass kama kwamba walicho kifanya ni sahihi. Tunakosea sana ...! Walioko kwenye ndoa ndio wanapaswa kupongezwa na si hivi. Tunaharibu vizazi vyetu,” Mwijaku alitema madini ya ushauri uliokolea.

Akitolea maoni yake binafsi kama yeye, alisema kwamba Nandy amewadhalilisha wqazazi wake na kumponda kwamba bora mara kumi angeliweka siri suala hilo na si kumshukuru Mungu hadharani kwa kitendo hicho alichokifananisha na ujinga.

“Mimi kwangu nitakwambia kua @officialnandy amewadhalilisha wazazi wake kwenye hili . Na ajue kua ameingia kwenye mifano ya wanawake watakao tolewa mifano mibaya ya ujana wakee. Viongozi wa dini mko wapi? Haya ndio mafundisho ya kondoo wa bwana? Tujitathimini wazazi. Tusiige kila ujinga. Alafu bora ungefanya siri sio unatangaza kabisa hadharani na unamshukuru mungu kweli? Kwa tendo hili. Hukupaswa kupost hukupaswaaaa,” aling’aka Mwijaku.

Nandy ambaye alionekana kumuelewa Mwijaku na utata wake hakulichukulia hili kwa umakini kwani alimjibu kimzaha zaidi akimtaka ashone suti yake ifaavyo isije ikambana siku ya harusi.

“Kwani hii dunia ni yetuuuuu hakikishaaa suit yako imenyoooka na isikubanee sanaaa maana misosi ni ya kutoshaaa @mwijaku,” alijibu Nandy kwa emoji za vicheko.

Juzi mwenyekiti wa shughuli ya harusi ya Nandy na Billnass alimtaja Mwijaku kuwa mmoja wa wanakamati ambao watashughulikia wageni watakaotoka upande wa bibi harusi ili kuhakikisha wanakulavizuri hadi wanasaza.