(Video) Rayvanny ajijengea heshima kuliko Harmonize, aondoka WCB kishujaa

Msanii huyo anaondoka baada ya kuanzisha lebo yake ya Next Level Music.

Muhtasari

• “Ndugu yangu Diamond Platnumz, heshima yangu kwako haitokaa ifutike, naudhamini sana mchango wako" - Rayvanny.

• "Ninakokwenda, nitawashika mkono vijana wengine kwa sababu pia mimi nilisaidiwa kufika hapa," - Rayvanny.

Baada ya kisia kisia za muda mrefu, hatimaye msanii Rayvanny ameondoka rasmi kwenye rekodi lebo iliyomlea na kumkuza kimuziki, WCB Wasafi.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Rayvanny ameushukuru uongozi mzima wa Wasafi ukiongozwa na mkurugenzi mkuu Diamond Platnumz na rasmi sasa kuondoka ambapo tayari alisha anzisha lebo yake kwa jina Next Level Music.

“Miaka 6 sasa tangu tumeanza kufanya kazi pamoja na hii timu yangu, familia yangu, WCB Wasafi. Upendo, umoja vimekuwa nguzo kubwa saba kama timu. Mengi nimejifunza lakini pia mengi tumefanikisha tukiwa pamoja,” alisema msanii huyo kwa sauti isiyo ya kufurahisha ya kuaga.

Rayvanny hakusita kuzungumzia baadhi ya mafanikio ambayo amepata akiwa kama mmoja wa familia kubwa ya WCB ambapo aligusia kwamba alifanikiwa kuwa msanii wa kwanza kushinda tuzo ya BET nchini Marekani na kuhimili kwa kutawala majukwaa mbali mbali ya kupakua na kusambaza miziki kama Boomplay.

“Shukrani za dhati kwa familia yangu Wasafi lakini pia kwa ndugu yangu Diamond Platnumz kwa kunipa nafasi dunia ione kipaji change nilichobarikiwa na mwenyezi Mungu ili kufika hapa nilipofika, kusaidia familia yangu na kufanikisha mengi katika maisha yangu,” Rayvanny alisikika akisema.

Kubwa zaidi ni kwa jinsi msanii huyo alimzungumzia bosi wake Diamond Platnumz ambapo alimshukuru pakubwa kwa kumuaminia miongoni mwa wasanii wengi na kumpa mkataba ndani ya pango la WCB  ambapo ndilo chupa lililomtoa na kumfahamisha kwa mashabiki wengi alio nao sasa.

“Ndugu yangu Diamond Platnumz, heshima yangu kwako haitokaa ifutike, naudhamini sana mchango wako Mungu akusaidie, na yote uliyonifanyia, Mungu akuzidishie,” aliongeza kusema Rayvanny.

Msanii huyo aliamua kutoka katika lebo ya Wasafi kwa njia moja ya kiheshima kimya bila kuzua mtafaruku kama ambavyo mwenzake Harmonize alifanya miaka mitatu iliyopita ambapo alizua tafrani na kukinukisha katika mitaa ya mitandaoni pakubwa huku akimdhihirisha Diamond kuwa mtu mbaya, jambo ambalo liliwakosanisha mpaka sasa.

“Ila naamini kwamba mtoto anayekuwa ni yule anayeondoka nyumbani kwenda kuanza maisha na kuiheshimu familia yake. Umenilea, umenikuza, sasa ni muda wangu wa kuondoka nyumbani na kuanza maisha mengine. Lengo ni ukuaji lakiji pia kuwapa nafasi vijana wengine, maana ninapotoka mimi, wengine wanapata nafasi ya kuingia lakini pia ninakokwenda, nitawashika mkono vijana wengine kwa sababu pia mimi nilisaidiwa kufika hapa,” alimaliza Rayvanny kwa sauti ya kuaga.