"Ukitaka kufaulu kimuziki mbali na WCB, anzisha bifu na Diamond" Rayvanny ashauriwa

Romanticx Aloyce aliwataja baadhi ya mastaa wanaoteleza katika utajiri kwa kuwa na bifu na Diamond na kumtaka Rayvanny kuwaiga.

Muhtasari

• “Rayvanny akibweteka atapotea aanzishe bifu na Diamond, awe anamzungumzia vibaya" mdau alishauri

• "Wote akina Mwijaku wamekuwa maarufu kwa sababu ya kumtukana Diamond,” Aloyce alisema

Diamond Platnumz na Rayvanny
Diamond Platnumz na Rayvanny
Image: HISANI

Mtangazaji na mchanganuzi wa mpira wa miguu nchini Tanzania Romanticx Aloyce amekuwa mtu wa hivi punde kutoa yake ya moyoni kuhusu kuondoka kwa msanii Rayvanny kwenye rejkodi lebo ya WCB Wasafi yake Diamond Platnumz.

Kulingana na Aloyce, Rayvanny atafifia kimuziki iwapo hatolazimisha kuzua ugomvi baina yake na aliyekuwa bosi na mlevi wake kimuziki, Diamond Platnumz.

Aloyce alisema kwamba Diamond ni kama chambo cha kukuza umaarufu kwani msanii yeyote anayetaka kuwa mkubwa basi sharti agombane au kuwa na bifu na Simba huyo wa Wasafi ili umaarufu wake kukua.

“Rayvanny hawezi kutoboa kimuziki kama hatoforce bifu na Diamond. Baada ya kuondoka WCB inatakiwa aiongelee vibaya Lebo hiyo. Msanii yeyote akiwa na Bifu na Diamond lazima awe msanii mkubwa. Rayvanny atumie akili asilazimishe bifu na Harmonize haitomsaidia aforce bifu na Diamond na awe rafiki wa Harmonize,” Aloyce alitoa maoni.

Mtangazaji huyo alisema kwamba anamuona Harmonize mtu wa kawaida tu kwani hajui kuimba na alikuwa anabebwa akiwa Wasafi lakini pindi alipotoka na kulizusha timbwiri na Diamond basi ndio umaarufu wake ulizidi kukolea.

Aloyce pia alisema hata Alikiba mwenyewe uimbaji wake ni wa kawaida sana na hana jipya kwenye gemu la bongo fleva lakini bifu lake na Diamond ndilo limemuweka kwenye anga za juu kimuziki.

“Harmonize hajui kuimba, hakuna achokifanya akiwa WCB alikuwa anabebwa na Lebo baada ya kuondoka WCB bifu na Diamond linambeba. Alikiba uimbaji wake ni wa kawaida, hatoi nyimbo nzuri lakini bifu na Diamond linamfanya aendelee kusikika. Wote akina Mwijaku wamekuwa maarufu kwa sababu ya kumtukana Diamond,” Aloyce alisema ukweli wake.

Kwa kutolea mifano ya wasanii hao wawili ambao bifu lao na Diamond ndilo linawabakisha kwenye muziki, amemtaka Rayvanny kufuata mkondo wao iwapo anataka kuzxidi kuwika mjini na vijijini.

“Rayvanny akibweteka atapotea aanzishe bifu na Diamond, awe anamzungumzia vibaya sana hapo atatoboa atasapotiwa na Wengi,” Aloyce alimshauri Rayvanny.

Ikumbukwe jana msanii na chawa wa WCB Baba Levo alimshauri Rayvanny kuilinda heshima yake na Diamond huko aendako mbali na WCB Wasafi kwa sababu msanii huyo ndiye aliyempa nafasi ya kusikika na watu wengi.

Juzi Rayvanny alipakia video yenye hotuba yake akiiaga familia ya Wasafi huku akimsifia Diamond pakubwa na kuahidi kuzidi kuilinda heshima yake kwake.