"Wasichana miaka 20-30 ukitongozwa kubali kuoleka, hisia zitakuja mbele ya safari" Mhubiri Beatrice

Aliwataka wanawake kutofanya mambo kuwa magumu kipindi wako bado wabichi wakifuata na wanaume.

Muhtasari

• "Wanaume wanatusikiliza sana, ukiongea hovyo mwanaume anajiambia tu huyu nikimuoa ataniua" - Mchungaji alisema.

Mchungaji Beatrice Byemanzi
Mchungaji Beatrice Byemanzi
Image: Instagram

Mhubiri mmoja kutoka nchini Uganda amegonga vichwa vya habari za umbea mitandaoni baada ya kuwataka watu, haswa wasichana wenye umri wa miaka kati ya 20-30 kukubali kuoleka na mtu yeyote kabla umri huo hujapita waanze kusema wanataka mtu yeyote bora anapumua.

“Unaona kati ya miaka 20-30, nataka kwanza kuzungumza na kina dada kwa sababu mimi ni mwanamke pia, kati ya huo umri wewe tayari ni bidhaa ghali sokoni, na hiyo dhana inaweza ikakuingia kichwani. Kubali kuoleka kipindi hicho kwa sababu ambacho hatutaki kitokee ni wewe kufika umri fulani uanze kusema Mungu jamani nataka mtu yeyote,” alishauri mhubiri huyo.

Alizidi kusema kwamba mambo mengine katika ndoa yatajipa tu kadri muda unavyosonga ukiwa katika ndoa, huku akitolea mfano kwamba yeye kipindi anaoleka na mumewe hakuwa na hata gari lakini walikuja kupata mali wakiwa pamoja katika ndoa.

“Hayo mambo mengine yanaweza kurekebishwa. Fedha zinaweza kurekebishwa, sura zao, kanuni za mavazi zinaweza kurekebishwa. Hayo sio mambo ya tabia, haswa mwanaume akiwa wa kuvutia, muoe haraka, hisia zitakuja,” alisema mchungaji.

Pia alisema kina dada wengi wanashindwa kupata wachumba kwa sababu wanaonekana kujichanganya mpaka wanaume hawapati kuwaelewa kwa ufasaha.

“Nimekuwa nikizungumza na baadhi ya vijana na wako na woga wa kuwafuata wasichana kwa sababu wasichana njia ambayo tunaongea, unajua ni vile ambavyo watakusikia, uko karibu naye na unaongea mambo mengi yenye ukakasi na yeye anasikiliza, atajiambia kimoyomoyo, huyu siwezi mjaribu, huyu kama nikimuoa ataniua,” mchungaji huyo alisema.

Mchungaji huyo kwa jina Beatrice Byemanzi pia aliwataka wanadada kutoingiwa na fikira ambazo wanaona wanaume wengine wakiwa nazo, kwamba kama waliona baba yao akiteseka na mama yao kwa uhaba wa kifedha basi na wao wanaona ndoa itakuwa ngumu kama ya wazazi wao.

Aliwataka kukubali ndoa na mtu yeyote hata kama hana mali bora upendo unaonekana huku akikashfu dhaan ya kutaka kukodisha magari mengi ili kufurahisha watu kipindi cha harusi.

“Mbona utumie laki tatu kwa magari ambayo huyamiliki ili kuendesha kwa saa mbili tu kufurahisha watu ambao baadae watakuja kukusema wakati uko katika mkwamo wa kifedha? Unajaribu kumfurahisha nani?” mchungaji Byemanzi aliuambia umati wa waumini kanisani.