(Video) "Cheni yangu inanunua kila kitu cha Khaligraph, saa inanunua fani ya sekula yote" - Ringtone

Ringtione alitangaza kugura rasmi sanaa ya injili na kujiunga miziki ya kidunia kwa lengo la kumng'oa Diamond.

Muhtasari

• Akionesha baadhi ya mapambo mwilini mwake, Ringtone alisema yote kwa ujumla ni ya thamani kubwa sana kuliko wasanii wote wa sekula.

Aliyekuwa msanii wa injili na ambaye sasa ndiye kipya kinyemi katika Sanaa ya miziki ya kidunia, Ringtone ametimiza ahadi yake kwa mashabiki wake aliyotoa kwamba pindi baada ya kuingia kwenye sekula basi atanunua macheni makubwa tena yenye bei ghali kama alivyo ghali mwenyewe.

Katika video moja ambayo imetembezwa mitandaoni, Ringtone ambaye awali alisema atabadilisha jina lake na kujiita Bringtone anaonekana akionesha macheni yake ghali na pete ambavyo vyote anavilinganisha na thamani ya baadhi ya wasanii kwenye fani ya sekula anaolenga kuwamwaga pindi atakapoachia madude yake ya kwanza kwenye sekta hiyo.

Msanii huyo mwenye mikogo mithili ya tausi anaonekana akisema kwamba cheni yake ya shingoni ni ya thamani ya milioni 7 pesa za Kenya na ya pili hajui thamani yake ila anachokijua ni kwamba itanunua kila kitu cha msanii Khaligraph na mpaka yeye mwenyewe.

“Hii cheni sijui bei ila ninachokijua ni kwamba inanunua gari la Khaligraph, inanunua nyumba ya Khaligraph, inanunua vitu vyote vya nyumba vya Khaligraph, na hizi pete mbili zinanunua maisha ya fasheni ya Willy Paul na hii moja ya almasi inanunua Diana B na Bahati kwa ujumla,” anaonekana akijishaua msanii Ringtone.

Pia alizidi kusema kwamba saa yake ya mkononi inanunua sekta ya miziki ya kidunia yote kwa jumla na kusema kwamba kwa jumla mapambo ambapo alikuwa ameyavaa mwilini mwake ni ya thamani kubwa isiyoweka kukadirika kwa takwimu za kikokotoo.

Ringtone alitangaza wiki mbili zilizopita kwamba amefika mwisho wa safari yake ya kuhubiri injili kupitia miziki na rasmi atakuwa anaanza ukurasa mpya katika fani ya miziki ya kidunia.

Msanii huyo anayejidai kuwa Tajiri zaidi ya wasanii wote nchini alisema sababu yake kuu kuachia injili ni kutokana na wanadada wengi kumfuata  na kumtongoza, jambo ambalo alisema linamvuta nyuma katika azma yake ya kuhubiri na ndio maana aliamua kuachia hata ngazi ya kuwa mwenyekiti wa wasanii wa injili ambacho ni cheo alichojiteua mwenyewe.