'Naumia ninapolinganishwa na mtoto' - Dorah

''Nitaelimisha watu , nitaonyesha watu kwamba binadamu aliyeumbwa na mwenyezi mungu anauwezo wa kukubadilisha'' Dora

Muhtasari

•Dorah ameshiriki michezo mingi ya tamthilia nchini Tanzania ikiwemo Kapuni na Juakali iliyozidi kumpa umaarufu.

•Hakuna dawa kamili kwa wagonjwa wengi wa Seli Mundu. Lakini tiba hutolewa ili kupunguza maumivu na kuzuia madhara yanayoweza kutokea kwa sababu ya ugonjwa huu. 

Dorah akiwa na aliyekuwa waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo, Innocent Bashungwa ambaye sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI
Dorah akiwa na aliyekuwa waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo, Innocent Bashungwa ambaye sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI
Image: INNOCENTBASH

Dorah akiwa na aliyekuwa waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo, Innocent Bashungwa ambaye sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI

Wanswekula Zacharia ndio jina halisi la msanii ambaye anajulikana na wengi nchini Tanzania kama Miss Dora .

Mwaka huu ametimiza miaka 27 na kwake yeye anasema kwamba ni muujiza kwamba yuko hai mpaka leo kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa Seli Mundu ama Sicke cell katika maisha yake ya utotoni , na hadi sasa anaishi na makovu ya ugonjwa huo .

”Nilipoanza kufahamu maisha nilijikuta kwamba sikuwa nakuwa kwa kimo kama watoto wengine , na hadi sasa muonekano wangu unaoneka nina mwili mdogo sana kuliko wanawake wa kawaida wa rika langu , Ila nimekubali jinsi nilivyo na ninajidhatiti kila siku kuyaishi maisha yangu kimamililifu”anasema Dorah .

Dorah ameshiriki michezo mingi ya tamthilia nchini Tanzania ikiwemo Kapuni na Juakali iliyozidi kumpa umaarufu.

Katika tamthilia ya Juakali, Dorah anasema kwamba alikubali, kuigiza katika nafasi ambayo inagusia maisha yake angalau kwa kiasi fulani  ili kudhihirishia ulimwengu mateso aliyopitia, kutengwa na kunyanyapaliwa.

”Kwa kweli sioni shida ikiwa watu wanaweza kujifunza kupitia maisha yangu halisi , kwani ninaamini kwamba itamuelimisha na kumpa matumaini angalau mtu mmoja ”anasema Dorah

Kwa sasa mwanadada huyu anatumia maumbile yake na kipaji chake sio tu katika uigizaji bali pia kutoa nasaha na kuwa kielelezo chema kwa watoto ambao wanazaliwa na mapungufu ya kimwili.

Nitaelimisha watu , nitaonyesha watu kwamba binadamu aliyeumbwa na mwenyezi mungu anauwezo wa kukubadilisha kwa mfano kunyanyapaliwa na jamii na wengi, lakini leo hii Dorah amesimama na amekuwa kama kioo katika jamii licha ya changamoto nyingi tu ” .

Kwa mujibu wa wataalam wa maswala ya Damu Seli Mundu ni tatizo la chembechembe nyekundu za damu la kurithi ambapo kunakuwa na upungufu wa chembechembe hizo za damu kwa ajili ya kusafirisha oksijeni kuzunguka mwili mzima.

Kwa kawaidi, seli nyekundu za damu zenye uwezo wa kunyumbuka husafiri kiurahisi ndani ya mishipa ya damu.

Mgonjwa wa Seli Mundu huwa na seli nyekundu zenye umbo la mwezi mchanga.

Seli hizi ngumu , zinazonata huweza kuziba mishipa midogo ya damu, hali ambayo huweza kusababisha damu kwenda polepole au kuziba mtiririko wa damu na oksijeni kuelekea sehemu nyingine za mwili.

Hakuna dawa kamili kwa wagonjwa wengi wa Seli Mundu. Lakini tiba hutolewa ili kupunguza maumivu na kuzuia madhara yanayoweza kutokea kwa sababu ya ugonjwa huu.