(Video) Kijana wa mjengo atokwa na machozi ya furaha kwa kupewa zawadi 10K na mwanamke asiyemjua

Mwanamke huyo alipakia video kwenye Instagram yake na mtu mmoja akajitolea kumpa 10K ili amkabidhi kijana huyo.

Muhtasari

• Baada ya kupakia video hiyo, mtu mwingine aliyeguswa alimtumia mwanamke huyo elfu 10 ili kumkabidhi kwa niaba yake

Mwanamke mmoja msamaria mwema amefurahisha nyoyo za watu wengi mitandaoni baada ya kupakia video akionesha ihnsani yake kwa kijana mmoja aliyekuwa akifanya kazi ya kufyatua matofali ya saruji.

Katika video alizozipakia kwenye ukurasa wake wa Instagram, mwakamke huyo kwa jina Ahuoiza alipakia video hiyo akikumbusha watu kwamba aliwahi ipakia wiki nane zilizopita na kuelezea vile alimkuta kijana huyo.

“Nilimuona kijana huyu akifanya kazi chini ya jua kali ndipo nikaamua kumpa mkono wa pole. Aliniambia nisijisumbue lakini nilisisitiza. Aliniambia jua litaharibu ngozi yangu lakini nikalazimisha kumsaidia,” mwanamke huyo aliandika kwenye video hiyo.

Baada ya kupakia video hiyo, mtu mwingine aliyeguswa alimtumia mwanamke huyo elfu 10 ili kumkabidhi kwa niaba yake. Ahuoiza aliwataka watu kujitokeza na kuwasaidia watu hata kama si kwa pesa bali kwa kuwaonyesha upendo tu.

“Ikiwa huna shughuli nyingi, nenda huko nje na onyesha upendo ❤️ kwa mtu leo. Huenda usiwape Pesa au zawadi. Unaweza kuwasaidia kwa chochote wanachofanya ili kupata riziki. Wafanye tu wahisi kupendwa,” aliandika kwenye instagram yake.

Katika video ya pili aliyopakia baada ya kumkabidhi kijana yule ile zawadi ya pesa aliyopewa na shabiki wa mwanamke huyo, kijana yule anaonekana kwenye video akifurahia mpaka kutaka kumsujudia kama ishara ya kupokea kwa shukrani tele.

Ishara hii ya upendo kutoka kwa mwanamke huyo ilitia joto nyoyo za wengi ambao walimpongeza kwa kuonesha upendo usiomithilika kwa watu hata asiowajua kamqa ishara moja ya kuwadhihirishia kwamba wanapendwa.

“Mungu wabariki watoaji wote. Na wewe hasa kwa dhana hii,” mmoja alimuandikia.