"Nilipewa 500K, nikajengea wazazi wangu nyumba kijijini" - Stevo Simple Boy

Msanii huyo alisema wasimamizi wake wa awali Made In Kibera walimpa nusu milioni kutoka kwa tangazo la OdiBet.

Muhtasari

• Simple Boy alisema usanii unalipa kama msanii ni mnyenyekevu na hana vituko vya kumharibia jina.

Msanii Stevo Simple Boy akiwa katika mahojiano na Mwafreeka
Msanii Stevo Simple Boy akiwa katika mahojiano na Mwafreeka
Image: YouTube Screenshot

Msanii wa moto kabisa sasa hivi nchini Kenya, Stevo Simple Boy amefichua kwamba wasimamizi wake wa awali katika kazi zake za muziki, Made In Kibera walimpa pesa nyingi sana baada ya maelewano ya kufanya tangazo la kampuni moja ya ubashiri humu nchini.

Akizungumza kwenye podcast ya aliyekuwa mtangazaji Mwafreeka, Simple Boy alisema kwamab Made In Kibera walimpa kiasi cha nusu milioni pesa taslimu za benki kuu ya Kenya na akafurahia sana ambapo alitumia kitika hicho kuwajengea wazazi nyumba.

“Kwa hiyo pesa nyingi kabisa ulipatiwa ukiwa huko, yaani umetumbuiza halafu ukapatia kwamab chukua hii, zilikuwa kiasi kipi?” Mwafreeka alimuuliza msanii huyo.

“Zilikuwa nusu milioni, kutoka kwa lile tangazo la OdiBet, nilipewa na kikajengea wazazi nyumba kijijini,” Stevo Simple Boy.

Aidha msanii huyo alipuuzilia mbali kauli kwamba usanii haulipi na kusema kwamba katika usanii kuna pesa iwapo msanii ako mnyenyekevu na hana vituko vingi vinavyomwandama na kulitia jina lake mchangani.

Msanii huyo anazidi kukwea ngazi za mafanikio tangu miezi michache walipotengana na aliyekuwa mpenzi wake, Pritty Vishy ambapo walimwaga mtama wa siri zao mitandaoni, kila mmoja akijaribu kulisafisha jina lake kwa kumkandia mwingine chini.

Hivi majuzi, Stevo Simple Boy alitangaza mipangi ya maisha yake na kusema kwamba hivi karibuni atafungua kampuni ya kutengeneza sharubati kwa jina Freshi Barida, jina ambalo amelitoa kwa wimbo wake uliomfanya kujulikana zaidi mwaka huu mpaka kubidi kufanya ‘remix’ ya ngoma hiyo akiwashirikisha wasanii wengine kutoka humu nchini.