"Sio vita vya ndugu, ni wivu wananionea!" Akothee afichua sababu ya ugomvi na ndugu zake

Akothee alitaka heshima kuchukua mkondo wake na kila mtu kuishia katika mlango wake.

Muhtasari

• "Sisi ni ndugu kwa bahati sio kwa hiari, lakini nachagua amani siku yoyote,” alirusha mkwara Akothee.

Msanii na mfanyibiashara Akothee akiwa nchini Ufaransa
Msanii na mfanyibiashara Akothee akiwa nchini Ufaransa
Image: Instagram//Akothee

Msanii Akothee amecharuka na kutema cheche kali kwa wanafamilia wake ambao inasemekana hawaonani jicho kwa jicho kwa kile kinachosemekana ni vita vya kuoneana wivu kwa mafanikio yake maishani.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Akothee alipakia picha yenye maneno makali na baadae akaisindikiza kwa cheche zingine huku akiwataka kila mtu kukaa kwenye mlango wake.

“Kweli kuna wale ndugu ambao watakuumiza kila wakati, kukusababishia maumivu na kuhisi kama hakuna kilichotokea. Wakome na wakome kabisa. Linda amani yako. Sijataja mtu,” Picha hiyo ilisheheni maneno hayo yaliyokuwa yanawalenga baadhi ya wanafamilia wake.

Vile vile alifuatisha kwa maneno ya lugha ya Dholuo ambao pia aliitafsiri kwa kusema kwamba ni wakati sasa kila mtu aishie kwa mlango wake. Pia alisema kwamba wao walijipata kuwa ndugu kibahati tu ila hakuna aliyechagua, na hivyo kuwataka ndugu zake wamkome kabisa.

“Kila mtu akae kwa mlango Yake, aishi maisha yake. Sisi ni ndugu kwa bahati sio kwa hiari, lakini nachagua amani siku yoyote,” alirusha mkwara Akothee.

Baadhi ya mashabiki wake ambao wamekuwa wakifuatilia maneno anayopakia kwenye kurasa zake mitandaoni walihisi hivi ni vita na dadake mdogo ambapo mmoja alijaribu kusema kwamba ni vita kwa kina dada wa toka nitoke lakini Akothee akamrekebisha na kusema ukweli wote huku akisema ni vizuri kitu kiitwe kwa jina lake bila kuficha.

“Hivi ni vita vya ndugu wa toka nitoke, na haswa wanawake,” shabiki kwa jina Imann Iman Faith aliandika.

“Hakuna kitu kama vita vya ndugu wa toka nitoke, huu ni wivu. Uite kwa jina lake bila kuficha,” Akothee aliandika.

Ikumbukwe hivi majuzi, Akothee aliwosia wanamitandao kwa maneno kwamba ni heri mtu kukaa mbali na familia kwani hawawezi kukusaidia na badala yake akawataka kuzoea kukaa na watu wasiowajua kwani hao wanaweza toa msaada mkubwa kuliko ambao familia inaweza toa.

Kwa sasa, mjasiriamali huyo yuko ziara ya kujivinjari nchini Ufaransa ambapo waliandamana na bintiye Rue Baby.