"Tukutane tarehe 22th" Rayvanny achekwa kwa kuboronga Kiingereza

Rayvanny amekuwa wa pili kuboronga kiingereza baada ya Diamond kusema miiaka 31st

Muhtasari

• Rayvanny aliandika kwenye Twitter akiwarai mashabiki wake kujumuika naye tarehe 22 akiachia ngoma mpya.

• Alichekwa kwa kuandika kiingereza cha 22th badala ya 22nd.

• Mapema mwaka huu Diamond pia alikuwa kicheko baada ya kudai ana miaka 31st.

Msanii Rayvanny akiwa na masikitiko baada ya kuchekwa Twitter
Msanii Rayvanny akiwa na masikitiko baada ya kuchekwa Twitter
Image: instagram//Rayvanny

Kwa mara nyingine tena, Wakenya wameendeleza mashambulizi yao ya mitandaoni dhidi ya Watanzania, kwa kile wanasema kwamba majirani hao hawana weledi katika lugha ya Kiingereza.

Hii ni baada ya picha kuibuka ya msanii Rayvanny akiwa ameandika Twitter kuwataka mashabiki wake kujumuiika na yeye Ijumaa iliyopita ambapo aliandika tarehe yake kama 22th badala ya 22nd.

Watu wengi walimshambulia Rayvanny kwa kubananga lugha hiyo ya mkoloni, huku idadi kubwa ikiwa ya Wakenya ambao wanajiona kama sungura katika weledi wa lugha hiyo ya kigeni.

Baada ya kushambuliwa vikali kwenye mtandao wa Twitter ambao nchini Kenya ni kama jukwaa rasmi la kuzua vita, Rayvanny ni kama alifuta Tweet ile kwani baadae watu kujaribu kuitafuta hawakuipata, lakini wengi walikuwa washaipiga picha.

Wakenya walimshambulia huku wengine wakisema alipoondoka lebo ya Wasafi aliacha Kiingereza huko huku wengine wakisema aliiga nyendo za aliyekuwa bosi wake Diamond Platnumz ambaye wakati mmoja pia alisikika akiboronga Kiingereza.

Mapema mwaka huu wakati wa uzinduzi wa filamu ya Netflix ya Young Famous and African, msanii Diamond Platnumz katika kipande kimoja aliulizwa ana miaka mingapi alijibu kuwa ana miaka 31st badala ya kusema thelathini na moja.

Hili pia lilizua mjadala mkali mitandaoni ikiongozwa na Wakenya waliomcheka vikali kwamba hajui Kiingereza.

Lakini je, kwa nini Wakenya wengi wanadhani weledi katika lugha ya mkoloni ni mafanikio makubwa maishani?

Kwa mfani, msanii Diamond wanayemcheka ni mmoja kati ya matajiri wakubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki, kwani tayari anamiliki lebo kubwa kabisa kuwahi kutokea katika ukanda huu, anamiliki kampuni ya habari pamoja ya kampuni ya kucheza kamari. Isitoshe, mwaka jana Diamond alinunua gari la kifahari la Rolls Royce ambalo hakuna hata msanii mmoja kwenye ukanda huu amewahi limiliki awali.

Kwa upande wake Rayvanny ambaye wanamcheka pia ni Tajiri kivyake kwani anamiliki lebo yake ya muziki ambayo tayari imemtoa kijana anayekuja kwa kasi za ajabu, MacVoice na pia ni msanii wa kwanza kutoka ukanda huu kuwahi kufikisha streams milioni 100 kwenye jukwaa la kupakua miziki la Boomplay.