"Jihathari dhidi ya watu, shabiki alinizawidi sabuni ikaniletea chunusi usoni" - Flaqo

Muigizaji huyo alisema alipewa zawadi ya sabuni na shabiki baadae ikamharibu uso vibaya mno.

Muhtasari

• Mashabiki mbalimbali walijitokeza na kutoa maoni yao kuhusu zawadi walizopatiwa na jinsi zilivyowaharibikia.

Muigizaji Flaqo411
Muigizaji Flaqo411
Image: Instagram//Flaqo411

Miaka miwili iliyopita, muigizaji wa klipu za kuchekesha akiiga sauti za watu katika familia, Flaqo alionekana na vimbimbi vingi usoni vilivyokuwa kama chunusi zilizojawa na uzaha, lakini msanii huyo amefichua kwamba zile hazikuwa chunusi za kiasili bali zilitokana na sabuni aliyopewa kama zawadi na mmoja wa wafuasi wake.

Akijibu maswali ya mashabiki wake kwenye Instagram yake, mmoja alimuuliza kama hatojali aeleze jinsi alivyotibu chunusi zile mpaka uso wake kurudi kuwa laini tena baada ya muda kupita.

Hapo ndipo Flaqo alifunguka kwamba zile hazikuwa chunusi bali ulikuwa ni ugonjwa wa Ngozi uliosababishwa na sabuni aliyoitumia, sabuni ambayo alidai kupewa na shabiki wake mmoja.

“Hazikuwa chunusi za kikweli, ilikuwa mwaka wa 2020 ambapo nilizawidiwa sabuni na mtu ambaye aliniambia ‘nataka kuwa shabiki’ sabuni hiyo ilikuwa na aside ya kojic ambayo ilichoma uso wangu vibaya sana na kuniacha na madoa meusi, ndio maana ghafla uso wangu ulikuwa na mabaka meusi, ila sasa niko vizuri ajabu,” Flaqo alisema.

Mashabiki mbali mbali walitolea maoni yao kuhusu zawadi walizopokezwa na watu waliojifanya kuwapenda na baadae zawadi hizo zikawageukia vibaya sana.

“Naapa wallahi hakikisha unawafahamu watu. Pia nilizawadiwa sabuni na "rafiki" kwa wiki kuelekea hafla yangu na wacha nikuambie Maina, uso wangu ulionekana kama chura baadaye. Asante Mungu kuna vipodozi! Bado ninapambana na mlipuko huo hadi sasa tangu Aprili,” alisema shabiki mmoja.

Wengine walimjia juu muigizaji huyo kwa kusema kwamba aside ile ndiyo ilimharibikia na kumwambia kwamba pengine haikuingiana na homini zake na wengine pia kumzomea kwamab alizawidiwa wala hakushrutishwa kutumia.

“Alikupa zawadi.. hakukulazimisha kutumia .. vitu viwili tofauti... Kutumia ilikuwa chaguo lako tu.. na kutaja shabiki hapa pia haina maana. Sema tu nilitumia sabuni ambayo iliniharibikia ....Mengine si muhimu,” shabiki mwingine alicharuka.