"Namtakia kila la kheri lakini hiyo ndoa haiwezi kudumu" - Mume wa kwanza wa Jeniffer Lopez

Jeniffer Lopezi alifunga ndoa kwa mara ya nne mwezi jana.

Muhtasari

• "Nilikuwa mume namba moja na aliniambia mimi ndiye mpenzi wa maisha yake. Tulipolala kitandani usiku wa arusi yetu, alisema tutakuwa pamoja milele’’ Ojani alisema.

 

Pete
Pete
Image: SERENDIPITY DIAMONDS

Mnamo mwezi jana, tarehe 18, mwanamuziki kutoka Marekani, Jeniffer Lopez aligonga vichwa vya habari baada ya kufunga ndoa yake ya nne na muigizaji Ben Affleck, miaka 20 baada ya kuahirisha mahusiano yao.

Licha ya mwanamama huyo kuvishwa pete kwa mara ya nne, ila bado aliyekuwa mume wake wa Kwanza Ojan Noa amesisitiza kwamba hata ndoa hiyo bado haitodumu kwani mwanamuziki huyo ana tabia ya kupoteza hamu ya ndoa haraka mno.

“Namtakia yeye na Ben kila la heri, lakini sina hakika kwamba itadumu. Jennifer anapenda kuwa katika mapenzi lakini amechumbiwa mara sita. Ben ni mume namba nne. Nilikuwa mume namba moja na aliniambia mimi ndiye mpenzi wa maisha yake. Tulipolala kitandani usiku wa arusi yetu, alisema tutakuwa pamoja milele’’ Ojani alisema.

Ojani walitengana na Lopez mnamo mwaka 1998 baada ya kudumu katika ndoa kwa mwaka mmoja ila wakabaki kuwa marafiki wakubwa, kinyume na mahusiano ya wengi ambayo pindi yanapovunjika basi ndio mwanzo wa uadui mkubwa mithili ya mwewe na kuku.

“Tulikuwa pamoja kimapenzi kwa miaka miwili lakini marafiki kwa karibu muongo mmoja, Tulipendana wakati tayari alikuwa maarufu. Lakini wakati wa ndoa yetu alikua megastar. Kwa miaka mingi ilikuwa chungu sana kuzungumza juu yake. Nilitaka kulala chini na kuishi maisha yangu. Lakini nilipoona ameolewa na Ben, ambaye ni kijana mzuri, hisia zilirudi,” alisema Ojani kulingana na jarida la Daily Mail.

Baada ya kutengana na Ojani mwaka 1998, mwaka 2001 Lopez tena alifunga ndoa na mwanaume mwingine kwa jina Cris Judd ambaye waidumu naye miaka michache kisha baadaye mwaka 2004 tena kwa mara ya tatu akafunga ndoa na mwanaume mwingine kwa jina Marc Anthony ambaye ni mtunzi wa nyimbo na pia muigizaji, kabla ya hii ya juzi na muigizaji Ben Affleck.