"Ukiwa na pesa Afrika unaishi vizuri kuliko matajiri wengi wa Marekani" - Rotimi

Rotimi ni msanii wa Kimarekani ambaye chembechembe zake zinatokea Nigeria.

Muhtasari

• Msanii huyo alionekana kupinga dhana kwamba Amerika kuna maisha mazuri kuliko Afrika kama ambavyo imekuwa ikisemekana kwa muda mrefu.

Image: INSTAGRAM// VANESSA MDEE

Rotimi ni Mmarekani mweusi ambaye ni Msanii na muigizaji wa kimataifa ambaye pia ni shemeji wa taifa la Tanzania kwa kumuoa mwanamuziki Vanessa Mdee.

Msanii huyo amezua mjadala mkali mitandaoni baada ya video fupi kuibuka ikimuonesha akisema kwamba ukiwa na pesa barani Afrika unaishi katika maisha mazuri mara kumi zaidi ya matajiri wa kutupwa na kuokotwa nchini Marekani.

Kulingana na Rotimi, mtu ukiwa na pesa ni kheri kuishi katika bara la Afrika kwani huku ni rahisi kupata amani na utulivu wa kiakili ikilinganishwa na Marekani ambapo Tajiri muda wote anaishi kwa mashaka kwa kuhofia maisha yake kwani huko takribani kila mtu anamiliki bunduki na visa vya ujambazi kwa kutumia bunduki hizo vipo juu sana kuliko bara lote la Afrika.

Rotimi alisema kwamab barani Afrika kuna mali bali nchini Marekani kuna utajiri na kusema kwamab hiyo ndio tofauti kubwa sana baina ya nchi yao na bara la Waafrika.

“Wakati uko na pesa Afrika haijalishi ni nchi gani, unaishi mara kumi zaidi ya watu wengi matajiri hapa Amerika. Kuna mali kule na sasa kuna utajiri huku, na hiyo ndio tofauti kubwa sana,” Rotimi anaonekana akizungumza pasi na kupepesa.

Bila shaka tamko hili la Rotimi linatofautiana na dhana ambayo wengi haswa Wakenya wamekuwa nayo tangu enzi za uhuru kwamba ukienda Marekani basi ndio mwanzo wa mwisho wa shida na matatizo yako kwani inasemekana huko maisha ni raha mstarehe.

Rotimi anasema ni kweli Marekani utajiri ni mwingi ila mtu mwenye mali yake hana furaha ya kuishi kama ambavyo wale weney mali yao barani Afrika wana amani ya nafsi kujiachia kwa mali na utajiri wao.

Ikumbukwe msanii huyo ambaye alimuoa mwanamuziki na aliyekuwa mtangazaji Vanessa Mdee baada ya kutengana na mwanamuziki Juma Jux, anasemekana kuwa na mizizi ya kiukooo kutoka taifa la Nigeria, nchi yenye idadi kubwa kabisa ya watu katika bara zima la Afrika.