'Rayvanny ameiheshimisha WCB ndani na nje ya nchi, hakustahili adhabu hiyo' Diamond asutwa

Kusuta huku kunafuatia madai kwamba Rayvanny alipigwa faini nzito kwa kutumbuiza tamasha lac Nandy Festival

Muhtasari

• "Lebo inafaa kuwa mtetezi wa wasanii na si mkandamizaji wa kukatisha tamaa za wasanii,” mwanamuziki Wakazi alifoka kwa uchungu.

Msanii Diamond Platnumz, na Rayvanny
Msanii Diamond Platnumz, na Rayvanny
Image: Instagram

Lebo ya WCB Wasafi imejipata katika vita vikali mitandaoni baada ya madai kuibuka kwamba ilimtosa msanii Rayvanny kima kikubwa cha faini kwa kile ilisemekana ni msanii huyo kuhudhuria tamasha la msanii Nandy lililofanyika wiki mbili zilizopita.

Mtangazaji wa Clouds Mwijaku alifichua kwamba hata baada ya Rayvanny kuweka wazi kuwa ameondoka Wasafi, ila bado hakuwa amekamilisha vipengee vyote vya kuondoka ili kuwa huru kabisa na moja ya sharti alilolikiuka ni kipengee kilichokuwa kikimtaka kutotumbuiza katika tamasha la msanii yeyote mshindani wa lebo hiyo kabla ya kuondoka rasmi, jambo ambalo anasemekana kulikiuka kwa kutumbuiza Nandy Festival.

Mwanzo alipoambiwa alipe milioni 800 ili aondoke, alikubali kulipa. Lakini kukawa na mvutano kuhusu akaunti zake za mitandao ya kidijitali. Wakawa hawajamalizana bado. Yeye alisimamisha malipo ya  800M zile ili kwanza wakubaliane kuwa akilipa pesa zile zote watampa akaunti zake zote za kidijitali. Wale wana utaratibu, ukienda kwenye disco/klabu ni milioni 5, ukienda kwenye tamasha la wazi 50M," Alisema Mwijaku.

Wiki jana Rayvanny alisemekana kuonekana katika makao ya muungano unaosimamia kazi za wasanii Tanzania, BASATA na sasa inadaiwa kwamba alikimbilia pale ili kupata usaidizi kutokana na faini hiyo ndefu aliyolimbikiziwa.

Wasanii mbalimbali sasa wamejitoa wazi na kumsuta Diamond pamoja na lebo yake kwa kile wamesema huu ni unyanyasaji mwingine zaidi ya ule wa lebo kuchukua 60% ya mapato ya kazi za wasanii.

“Rayvanny amewaheshimisha WCB Wasafi nchini na duniani kote. Ameshiriki tuzo za MTV, amefanya collabo za kimataifa, ameshinda tuzo ya BET miongoni mwa heshima nyingine nyingi za mafanikio. Kwa heshima hii, alikuwa anawadai kuondoka huru bila kulipia chochote na si kumchezea mchezo mchafu na kumkandia kama ambavyo wanamfanyia. Alilipa madeni yake! Lebo inafaa kuwa mtetezi wa wasanii na si mkandamizaji wa kukatisha tamaa za wasanii,” mwanamuziki Wakazi alifoka kwa uchungu.

Msanii huyo wa kuchana aliendelea kukemea kitendo cha Wasafi ambapo alisema kwamba hata lebo ya kimataifa kwenye miji ya watu kule Marekani Shady, Aftermath na Interscope zilikuwa kwa kipindi kimoja na msanii 50 Cent ila alipotoa albamu ya Grodt ambayo ilifanya vizuri zaidi ya maelezo, ilibidi lebo ile irudi kwenye mkataba na kuutathmini vizuri ili kumlipa 50 Cent alichokuwa anastahili kwa kuwa aliwaheshimisha kote ulimwenguni.