Diamond Kutumbuiza Nairobi Agosti 6

Msanii huyo alitumbuiza kwenye hafla rasmi ya Koroga Festival Nairobi mara ya mwisho Februari 2020.

Muhtasari

• Diamond alitangaza kupitia Instagram yake ratiba yake huku akiipatia Nairobi kipaumbele wikendi hii na kufuatisha tamasha zingine Canada na mwishoni wa mwezi huu wa Agosti.

Msanii Diamond Platnumz
Msanii Diamond Platnumz
Image: Instagram//DiamondPlatnumz

Msanii namba moja wa muda wote katika ukanda wa Mashariki ya Afrika, Diamond Platnumz ametangaza kwamba Jumamosi ya tarehe 6 Agosti atakuwa na tamasha la kutumbuiza nchini Kenya, tangu mwaka wa 2020 alipotumbuiza rasmi katika hafla ya Koroga Festival.

Diamond ambaye kwa mara nyingi amekuwa akiingia Kenya kisiri kwa kile kinasemekana ni kuenda kumuona mtoto wake Naseeb Junior ambaye walizaa na mzazi mwenziwe mwanamuziki Tanasha Donna, hajawahi kutumbuiza hadharani kwa miaka miwili sasa na ujio wake huu utakuwa wa kipekee kwa mashabiki wake wa Kenya kupata upenyo wa kuionja EP yake ya FOA ambayo anaendelea kuinadi katika pembe zote za dunia.

Wiki iliyopita, Diamond alikuwa na tamasha kubwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo umati ulishona kumsubiria Simba huyo anayenguruma kutoka mashariki mwa Afrika.

Hii ni baada ya kurejea kutoka Ulaya alikokuwa kwa takribani majuma matatu akizuru mataifa mbali mbali kama vile Ubelgiji, Ufaransa na Ujerumani akiinadi EP yake kwa wazungu ili kuipatia umaarufu zaidi si tu Afrika bali katika kanda ya dunia yote.

Diamond alitangaza kupitia Instagram yake ratiba yake huku akiipatia Nairobi kipaumbele wikendi hii na kufuatisha tamasha zingine Canada na mwishoni wa mwezi huu wa Agosti.

Diamond amejiandaa kuja Kenya wakati ambapo taifa hili linajiandaa kuelekea uchaguzi mkuu mapema wiki kesho, na wengi wameizungumzia tamasha hii ya Diamond kama moja ya kunadi na kuhubiri amani miongoni mwa vijana ambao ndio asilimia kubwa ya mashabiki wake nchini, dhidi ya kujihusisha na visa vya vurugu kabla, wakati na baada ya uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Agosti 9.