“Alfajiri njema, nguvu mpya na safari inaendelea,” Willis Raburu asema baada ya kunyoa rasta

Raburu ana umaarufu kutokana na kipindi chake cha runingani cha 10Over10

Muhtasari

• Willis Raburu anajiunga na wengine walionyoa rasta kama Nick Odhiambo, Thee Pluto, Magix Enga, Sean Andrew miongoni mwa wengine.

Mtangazaji Willis Raburu katika muonekano mpya bila rasta
Mtangazaji Willis Raburu katika muonekano mpya bila rasta
Image: Willis Raburu//Facebook

Mtangazaji maarufu nchini, Willis Raburu hatimaye amezikata rasta zake alizodumu nazo kwa takribani miaka mitatu.

Katika picha ambayo aliipakia kwenye ukurasa wake rasmi wa Facebook, kinara huyo wa kipindi cha runingani cha 10Over10 alipakia picha hiyo huku akidokeza kwamab ndio tena amerudi mwanzo kuanza upya na kusonga mbele.

“Alfajiri njema, nguvu mpya na safari inaendelea,” Willis Raburu aliandika kwenye picha hiyo ambayo aliiweka kama utambulisho wake kweney mtandao wa Facebook.

Mashabiki wake walimsifia kwa muonekano huo mpya huku wakimuambia sasa anaonekana kaboreshwa na utanashati hata zaidi kuliko awali alipokuwa na chokodindo hizo kichwani.

Wengine wenye dhana ya kuhusisha rasta na dawa ya kulevya ya bangi walimwambia kwamba sasa ako vizuri na Wajackoyah amemtoka kichwani, kwa maana kwamba wakili msomi George Wajackoyah anayegombea urais ameupa upanzi na ukuzaji wa bangi kipaumbele katika manifesto yake.

“Muonekano ni mwepesi bila Dreadlocks, Wajakoyah ametoka kichwani mwako,” shabiki wake kwa jina Mitch Marya alimuambia.

“Yaani uliamua kuangusha Wajackoyah chini hivo tu!” mwingine kwa jina Tasha Baibe alimtania.

Raburu sasa anajiunga kweney orodha ndefu ya watu maarufu waliotangaza kuasi chama cha rasta akiwemo mtangazaji mwenye sauti nzito Nick Odhiambo ambaye alikuwa mpenzi wa nywele hizo kwa muda mrefu lakini miaka michache iliyopita akawashangaza wengi baada ya kuibuka na muonekano mpya wa nywele fupi.

Mjukuu wa rais wa tatu hayati Mwai Kibaki, Sean Andrew pia naye mapema mwaka huu kabla ya kifo cha babu yake alitangaza kuzinyoa rasta zake kwa kile alisema kwamba ni watu walikuwa wanamhusisha na dhana mbaya inayohusisha wapenzi wa rasta na visa hasi katika jamii kama kutumia bangi na kuhusishwa na magenge ya uhalifu kama Mungiki.

Wiki chache zilizopita pia mtayarishaji wa muziki wa gengrtone maarufu nchini Kenya, Magix Enga alipakia video kwenye ukurasa wake wa Instagram akisema kwamab ameamua kuachana na ufugaji wa nywele ndefu na ni wakati sasa wa kufanya kichwa kiwe laini bila hata mzizi mmoja wa nywele.

Katika orodha hiyo, Raburu pia anakutanqa na mkuza maudhui Thee Pluto ambaye naye aisema alizinyoa baada ya kuahidiwa kiasi cha pesa fulani na rafiki wake.