"Wanasiasa walioshindwa na kukubali ni mashujaa usiwacheke, jifunze!" - Ezekiel Mutua

Mutua amewapongeza wote walioshindwa na kukubali matokeo ya uchaguzi nchini Kenya.

Muhtasari

• "Koja la maua kwa kila mtu ambaye ameonyesha ukuu huu wa roho!” Mutua alisema.

Mkurugenzi mkuu wa chama cha hakimiliki za muziki Kenya, MCSK Ezekiel Mutua
Mkurugenzi mkuu wa chama cha hakimiliki za muziki Kenya, MCSK Ezekiel Mutua
Image: Facebook//EzekielMutua

Mkurugenzi mkuu wa chama cha hakimiliki ya muziki cha kenya MCSK, Ezekiel Mutua amekuwa katika mstari wa mbele kipindi hiki cha kuhesabu na kutangazwa kwa matokeo ya chaguzi kuwapa wakenya wosia jinsi ya kujiweka watayarifu na matokeo yoyote.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Mutua amekuwa akiwahimiza Wakenya kuendeleza kudumisha amani huku nchi ikisubiri tume huru ya mipaka na uchaguzi IEBC kutangaza rasmi matokeo ya uchaguzi wa urais ambayo mchakato wa kuhesabu kura hizo yanaendelea katika kituo kikuu cha kuhesabu kura cha Bomas jijini Nairobi.

“Wapendwa Wakenya, itachukuwa muda mrefu kabla ya kupata tangazo la mwisho kutoka kwa IEBC kuhusu nani atakuwa Rais ajaye. Kwa sasa endelea na maisha yako ya kawaida na tusubiri neno la mwisho la IEBC Jumatatu ya hivi punde!,” Mutua alisema.

Pia msomi huyo aligusia suala la wanasiasa mbali mbali ambao wameonesha ukomavu kwa kukubali matokeo pindi wanapogundua kwamba wameshindwa katika nyadhifa mbali mbali walizokuwa wakiangazia macho.

Mutua alisema kwamba huo ni ukomavu wa kidemokrasia ambao umeanza kuonekana kweney tasnia ya siasa za Kenya na kuwapongeza huku akiwataka Wakenya kutowacheka wale wanaoangushwa bali kutumia fursa hiyo kama funzo.

“Ukiona wanaume wanaanguka, usicheke. JIFUNZE! Mashujaa wa kweli wa uchaguzi huu ni watu ambao ni wakubwa kwa kushindwa na wametangulia kukubali na kuwapongeza wapinzani wao. Inachukua ukomavu kufanya hivyo. Koja la maua kwa kila mtu ambaye ameonyesha ukuu huu wa roho!” Mutua alisema.

Huu ndio uchaguzi wa kwanza ambao umewaona wanasiasa mbali mbali kuangushwa na kukubali matokeo hata kabla ya IEBC kutoa matokeo rasmi na hili limeshabikiwa na wengi kama ishara ya kuonesha ukomavu wa kidemokrasia ya siasa za Kenya.