Mmishonari Mmarekani Anayezungumza Kiswahili Akiri Kutoamini Katika Biblia Tena

Justine Bradford ni Mwamerika alikuwa akihubiri injili nchini Kenya kwa Kiswahili.

Muhtasari

• "Si ati nilikuwa nimeamini kwa moyo, ilikuwa ni wazazi, nilikuwa nafanya hivyo ili kuwafurahisha wazazi na familia, lakini mimi mwenyewe sikuwa nimeamini,” Justine Bradford alisema.

Justine Bradford, mmishonari aliyekuwa akihubiri Kenya
Justine Bradford, mmishonari aliyekuwa akihubiri Kenya
Image: Screengrab//MkenyaMarekaniTV

Wengi ambao ni wafuatiliaji wakubwa wa kipindi cha ucheshi cha Churchill bila shaka wanamjua ama wamewahi kusikia na kumuona jamaa mmoja mzungu ambaye anazungumza Kiswahili na Kikuyu kwa wepesi mno. Jamaa kwa jina Justine Bradford.

Bradford alipata umaarufu wake nchini Kenya wakati alialikwa kuchekesha katika Churchill Show ambapo aliwavunja mbavu Wakenya kwa weledi wake katika lugha ya Kiswahili na Kikuyu.

Mzungu huyo mwenye asili ya Marekani alisema kwamba alikuwa nchini Kenya kwa miaka miwili tu na dhumni lake kubwa lilikuwa ni kuhubiri injili na kuwafunza Watu neno la bwana, yaani kama Mmishonari.

Lakini cha ajabu ni kwamba, juzi kati katika mahojiano na mkuza maudhui mmoja kutoka Kenya mwenye makaazi yake Marekani, Mkenya Marekani, Bradford alisema kwamba alishaacha kuhubiri injili na wala haamini tena katika hilo.

“Kenya nilikuwa mmishonari kuwafunza watu kuhusu Biblia na Ukristo ila kwa sasa sifanyi hivyo tena, niliacha kuamini na ukweli ni kwamba hata hapo awali sikuwa nimeamini, si ati nilikuwa nimeamini kwa moyo, ilikuwa ni wazazi, nilikuwa nafanya hivyo ili kuwafurahisha wazazi na familia, lakini mimi mwenyewe sikuwa nimeamini,” Justine Bradford alisema.

Mzungu huyo alizungumzia kwamba Kenya kitu kilikuwa tofauti kabisa ni vumbi katika maeneo mengi tofauti na nyumbani kwao Marekani na kuwashauri watu kutokuwa na uchu wa kuenda Marekani kwani ni kitu kilichochagizwa katika akili za Waafrika wengi kwamba Marekani ndio nchi nzuri kote ulimwenguni.