NPS yamsherehekea koplo Purity mwenye talanta ya ushairi, kucheza soka

Koplo Purity Nekesa ni afisa wa polisi ambaye ni mahiri katika ushairi, uchezaji kandanda, dereva, mama na mke wa mtu.

Muhtasari

• Yeye ni mmiliki wa Tuzo ya Utumishi Uliotukuka iliyotolewa na Inspekta Jenerali wa Polisi.

Koplo Purity Nekesa akiwa kama afisa wa polisi na mchezaji wa Harambee Starlets pia
Koplo Purity Nekesa akiwa kama afisa wa polisi na mchezaji wa Harambee Starlets pia
Image: NPS//Facebook

Tume ya hudumu ya kitaifa kwa polisi NPS Ijumaa lilimtambua mmoja wao na kumsherehekea kwa kuwa na uwezo wa kufanya mambo mbali mbali kando na kuhudumia taifa kwenye magwanda ya polisi.

Afisa wa polisi Purity Nekesa Muraya ni mwanasoka, mshairi, dereva, mama, na mke ambaye amefanya vyema katika Huduma ya Kitaifa ya Polisi. Yeye ni mmiliki wa Tuzo ya Utumishi Uliotukuka iliyotolewa na Inspekta Jenerali wa Polisi.

Na wakati Harambee Starlets, Timu ya Kitaifa ya Kandanda ya Kenya, ilipokonga nyoyo za Wakenya kupitia ushindi wake wa kuvutia kimichezo, Koplo Purity alikuwa miongoni mwa wachezaji muhimu katika timu hiyo. Ameiwakilisha nchi kimataifa katika Nigeria, Rwanda, Tanzania, Uganda, na Burundi.

Afisa huyo mrembo ana Stashahada ya Ushauri wa kisaikolojia na Maendeleo ya Jamii kutoka Chuo Kikuu cha Zetech. Yeye ni mhitimu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Wiyeta na Shule ya Msingi ya Kipsaina. Ni kutoka kwa taasisi hizi kuu ambapo fadhila za bidii, nidhamu, heshima, unyenyekevu, na huruma zilipandikizwa na kukuzwa ndani yake.

Koplo Purity Muraya aligundua weledi wake katika ushairi akiwa bado katika shule ya msingi. Alikuza kipawa chake katika shule ya upili na alionyesha ujuzi wake kikamilifu kupitia maonyesho ya kupigiwa mfano katika matukio kama vile harusi, siku za kuzaliwa, na matukio ya kidini wakati wa likizo za shule.

Mshairi huyo mashuhuri anapokea usaidizi mkubwa kutoka kwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi ambayo imemfanya apate umaarufu wa Kitaifa na kimataifa. Amepata fursa ya kutumbuiza katika shughuli za ngazi ya juu za polisi na kuwatumbuiza wageni wa ndani na nje ya nchi katika hoteli mbalimbali za nyota tano. Zaidi ya hayo, anahusika sana katika wimbo unaoitwa 'NPS Anthem' ulioimbwa na Mandilly.