Ommy Dimpoz ajigamba baada ya kukutana na kikosi cha Manchester United, kutambuliwa na klabu

United ilipakia picha ya staa huyo wa Bongo akiwa amevalia jezi ya klabu kwenye Instastori.

Muhtasari

•Jumatatu jioni mwanamuziki huyo alikuwa Old Trafford na alishuhudia Mashetani Wekundu wakiwalima Liverpool 2-1.

•Picha yake na Ronaldo ndiyo iliyoteka  umakini wa wanamitandao wengi huku maelfu wao wakiingiliana nayo.

Image: TWITTER// OMMY DIMPOZ

Staa wa Bongo Ommy Dimpoz ameeleza furaha yake kubwa baada ya kupata nafasi kutembelea uwanja wa Old Trafford nchini Uingereza na kukutana na baadhi ya wachezaji wa klabu ya Manchester United.

Jumatatu jioni mwanamuziki huyo alikuwa Old Trafford na alishuhudia Mashetani Wekundu wakiwalima Liverpool 2-1.

Baada ya mechi, Dimpoz aliweza kukutana na baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo anayoshabikia wakiwemo mshambulizi Christiano Ronaldo, kiungo Bruno Fernandes, beki Eric Baily, na mlinda lango David de Gea.

"Mtanzania wa Kwanza kualikwa rasmi na @ManUtd na kupiga picha na Wachezaji woteeee kama yupo mwingine niite Mbwa nimekaa paleeee," Dimpoz alisherehekea kwenye Twitter.

Alisindikiza ujumbe huo wake na picha kadhaa akiwa na baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza cha United.

Picha yake na Ronaldo ndiyo iliyoteka  umakini wa wanamitandao wengi huku maelfu wao wakiingiliana nayo.

"Namsaidia Mama Kuitangaza Tanzania 😁 Mkiniona na @B_Fernandes8 Zanzibar kuweni wapoleeee," Aliandika chini ya picha yake na Bruno Fernandes.

Dimpoz pia alipakia video yake na kipa David De Gea na chini yake kumtambua kama mlinda lango bora zaidi duniani.

Chini ya video yake na Bailly, mwanamuziki huyo alimtakia kheri beki huyo wa Ivory Coast anapojiunga na Marseille kwa mkopo.

"Maisha ni Connection @MwanaFA Alinitambulisha kwa Eric ALAFU Eric akanitambulisha kwa Timu nzima hata mimi ukitaka kupiga picha na Mayele Connection nnayo 😁 njoo ofisini kwangu GSM," Alisema.

Kufuatia ushabiki wake mkubwa kwa klabu,  Machester United iliweza kumtambua Dimpoz kupitia kwenye ukurasa rasmi wa Instagram.

Image: INSTAGRAM// OMMY DIMPOZ

United ilipakia picha ya staa huyo wa Bongo akiwa amevalia jezi ya klabu kwenye Instastori za akaunti rasmi ya klabu.

"Mtanzania wa Kwanza kupostiwa kwenye page ya Insta ya @ManUtd 😁 kama nawaona mnavyokimbilia kuhakikisha," Alisherehekea.

Dimpoz ambaye kwa sasa yupo Uingereza ni  mmoja wa wasanii ambao ni mashabiki sugu wa Mashetani Wekundu.