Mpaka ninakufa, Siwezi sahau jinsi familia ilinitenga, ila nimesamehe - Abdul, Babake Diamond

Nimesamehe. Niko na amani na sina dukuduku lolote katika moyo wangu kwa mtu yeyote aliyenikosea - Mzee Abdul.

Muhtasari

• “Kusema kweli vitu ambavyo vilinitokea katika maisha yangu tangu niko kijana mpaka umri huu wa ukubwani vitu vingi vilitokea vibaya" - Mzee Abdul.

Mzee Abdul amesema amesamehe Bi Sandra na wanawe kwa kumtenga
Mzee Abdul amesema amesamehe Bi Sandra na wanawe kwa kumtenga
Image: Instagram, YouTube screengrab

Abdul Juma Isack Luninze, baba wa kumzaa msanii maarufu wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz kwa muda mrefu amekuwa akizungumziwa kuwa na matatizo chungu nzima licha ya mwanawe kunukia na kuogelea kwenye utajiri.

Mzee Abdul ambaye juzi kati alifanya mahojiano ya kugusa sana na chaneli moja ya YouTube alifunguka makubwa kuhusu safari yake ya maisha, na kubwa tangu familia yake, kwa maana ya Diamond na ndugu zake pamoja na mama yao Sandra walipomtenga mzee huyo.

Alifichua kwamba kwa muda mrefu amekuwa akiugua saratani ya Ngozi, tatizo ambalo limemkwamiza katika mishe nyingi huku akipitia changamoto si haba katika kutafuta matibabu ya mionzi.

Mzee huyo pia asingemalizia mahojiano hayo bila kubeta kidogo kugusia matukio ya nyuma yaliyoisambaratisha familia yake – Familia ambayo aliitaja kuwa alikuwa anaitegemea sana kabla ya ufa kuingia kati yake na Bi Sandra – Mamake Diamond Platnumz.

Licha ya kila mtu kujua kwamba mzee Abdula ndiye baba wa kumzaa Diamond pamoja na nduguze, Mama Dangote mwaka jana aliweka wazi katika vyombo vya habari akisema kwamba Abdul siye baba halali wa watoto wake.

Mzee huyo alisema kwamba jambo hilo lilimuuma sana kwa kweli na kulitaja kuwa tukio moja katika maisha yake ambalo katu hawezi kulisahau kabisa mpaka anakufa na kurudi mchangani.

“Kusema kweli vitu ambavyo vilinitokea katika maisha yangu tangu niko kijana mpaka umri huu wa ukubwani vitu vingi vilitokea vibaya na vingine vizuri, ila kuna moja ambalo siwezi kulisahau. Kuja kutolewa katika familia ambayo nilikuwa nategemea, kusema kweli sitoweza kusahau kusema kweli kwa muda mrefu mpaka kufa kweli sitolisahau,” Mzee Abdul alieleza baina ya majonzi.

Mzee huyo ila alisisitiza kwamba yeye hana kinyongo na familia yake iliyomtenga – kwa maana ya Bi Sandra na wanawe kina Diamond na wengine.

Alisema kwamba ameshasamehe kabisa kwani hata yeye alisamehewa na wazazi wake na katu hawezi kulibeba kovu hilo moyoni hata ingawa hawezi kusahau tukio lile mpaka anakufa.

“Suala la kusamehe linakuja kwetu binadamu, vitabu vya dini vinatufunza kusamehe. Nikiwa kama mzazi ambaye ni muelewa, na mimi mwenyewe vile vile nimewahi kusamehewa hapo nyuma na wazazi wangu. Mimi kusamehe kwangu ni kitu chepesi, mimi ni mtu mwepesi wa kusamehe, nimesamehe,” Abdul Juma Isaac Luninze, babake Diamond alitamka.

Alitoac sababu ya kusamehe kwake kwa kusema kwamba siku zote kama mzazi mlezi, mtoto akikunyea kiganjani huna haja ya kikikata bali unanawa tu na kila kitu kingine kinaendelea mbele.

“Kama kuna mambo yaliyonitokea katika nafsi yangu nimesamehe kwa moyo mmoja, hata nikiingia katika ardhi ya Mwenyezi Mungu, mimi nimesamehe kabisa kama Mungu anavyosamehe. Niko na amani na sina dukuduku lolote katika moyo wangu kwa mtu yeyote aliyenikosea,” Mzee alisisitiza msamaha wake kwa familia yake iiyomtenga.

Alisema kwamba tayari ashakuwa mtu tofauti na ameanza maisha yake mapya bila familia yake licha ya kuendelea kusumbuliwa na tatizo la saratani ya Ngozi ambalo alisema linakuna na Kwenda kwa misimu.