Siku ya Alhamisi staa wa Bongo Ali Saleh Kiba alilazimika kuahirisha ziara yake ya muziki ya Marekani kutokana na masuala ya kiafya.
Katika taarifa ambayo alitoa kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Kiba alisema kuwa uamuzi wa kuahirisha ziara ya 'My Only One King Us Tour' ulijiri baada ya kugundulika kuwa na maradhi ya Covid-19.
"Kwa hili tunalazimika kuahirisha na kupanga upya hadi tarehe nyingine ya hivi punde kama iwezekanavyo. Hakuna kitu muhimu zaidi kwangu kuliko afya ya bendi yangu, wenzangu na ninyi mashabiki wangu," Kiba alisema.
Ziara ya 'My Only One King Us Tour' ilitazamiwa kung'oa nanga leo Ijumaa, Septemba 2 na kuendelea hadi Oktoba 1, 2022.
Kufuatia kuahirishwa kwa ziara hiyo, Kiba amewaomba radhi mashabiki wake ambao walikuwa wameisubiri kwa hamu kwa usumbufu uliojitokeza.
"Hadi wakati huo natumai kila mtu atakuwa salama na kuchukua tahadhari zote muhimu. Inshaallah tutaonana hivi karibuni," Mwimbaji huyo aliwaambia mashabiki wake.
Bosi huyo wa Kings Music Records alitazamiwa kuanza ziara yake siku ya Ijumaa katika mji mkuu wa Marekani, Washington DC.
Jumamosi alitarajiwa kutumbuiza jijini Minneapolis katika jimbo la Minnesota na baadae kufanya shoo jijini Kansas siku ya Jumapili.
Ratiba yake kwa kipindi cha ziara kilichobaki ilikuwa kama ifuatavyo:-
Septemba 10- Des Moines, Lowa
Septemba 16- Atlanta, Georgia.
Septemba 17- Lexington, Kentucky
Septemba 23- Manchester,New Hampshire
Septemba 24- Chicago, Illinois
Septemba 30- Los Angeles
Oktoba 1- Houston, Texas.
Kisa cha kwanza cha COVID-19 kiliripotiwa kwa mara ya kwanza katika jiji la Wuhan, Uchina, tarehe 31 Desemba 2019.
Nchini Tanzania, kisa cha kwanza kiliripotiwa jijini Arusha mnamo Machi 16, 2020 kabla ya kusambaa katika maeneo mengine.