(+video) Nitaanza kuiga Rachael Ruto kuombea mume wangu na ndoa yangu - Esther Musila

Ninajivunia sana na nitaenda kumuiga - Musila.

Muhtasari

• Tunapopiga magoti kama wake kuwaombea waume zetu, hilo ndilo linalowaweka pamoja - Musila.

Esther Musila, mkewe mwanamuziki Guardian Angel amewataka wanawake kuwaombea mabwana zao kila muda na kila siku ili kudumisha ndoa zao kwani ndoa nzuri ni ile yenye misingi kwa Mungu.

Akizungumza na blogu ya SPM Buzz, Musila alisema kama kuna kitu kimoja amejifunza kutoka kwa mama Rachael Ruto, mkewe rais mteule wa tano William Ruto, ni kuweka ndoa katika maombi na haswa kumpa mume wake sapoti katika maombi.

Musila alisema kwamba kitu amabcho kilimfanya Ruto kushinda majaribu yote amabyo ilikuwa inaonekana serikali yake ya Jubilee ilimgeuka na kila kitu kikaonekana kuenda kinyume na yeye, mpaka kuibuka mshindi katika kinyang’anyiro cha urais ni maombi ya mkewe mama Rachael Ruto.

“Mimi kama kuna kitu nimejifunza kutoka kwa mama Rachael Ruto ni kwamba sisi kama wanawake, tuwaombee waume zetu. Tunapopiga magoti kama wake kuwaombea waume zetu, hilo ndilo linalowaweka pamoja. Inashikilia familia na taifa. Ninajivunia sana na nitaenda kumuiga. Nitamuombea mume wangu, nitapiga magoti na kumwombea kila siku,” Musila alisema.

Musila alisema kwamba anajivunia sana Rachael na kumtaja kama mtu ambaye atakuwa anamwiga kila siku katika kuiombea ndoa yake na mwanamuziki Omwaka, almaarufu Guardian Angel.

Alikuwa akizungumza huku wakiwa wameshikana mabega na mumewe ambaye alikuwa ametega sikio pasi na kusema lolote.

Musila na Guardian Angel wamekuwa wakishtumiwa katika mahusiano yao haswa kutokana na dhana kwamba wametofautiana pakubwa kiumri, Omwaka akiwa na miaka takribani 30 huku Musila akiwa na miaka 50 na ushee.

Wengi wamekuwa wakiwashinikiza na kuwasimanga kwamba ndoa yao haitodumu kutokana na umri uliokwenda wa Musila kwani katika kisayansi, hatowezac kumzalia Angel mtoto.

Ila wawili hao katika mahojiano ya awali walinukuliwac wakisema kwamab mahusiano yao hayazingatii sana kigezo cha ujio wa mtoto kwani kikubwa ni mapenzi na kama mtoto atakuja mbele ya safari basi itakuwa kama nyongeza.

Angel na Musila walifunga ndoa ya faragha mwishoni mwa mwaka jana na wamekuwa wakiishi pamoja kaam mke na mume.