Ukitaka kufanikiwa, oa mwanamke mfupi, ukioa mrefu ataiba nyota yako - Ringtone

Ringtone alitolea mfano wa picha ya marais Uhuru Kenyatta na William Ruto pamoja na wake zao.

Muhtasari

• "Wanawake warefu kuwaliko wataiba nyota ya mafanikio yenu,” Ringtone alishauri.

Ruto awashauri wanaume kujifunza kutoka kwa marais wawili, kuoa wanawake wafupi
Ruto awashauri wanaume kujifunza kutoka kwa marais wawili, kuoa wanawake wafupi
Image: Instagram//Ringtone Apoko

Aliyekuwa mwanamuziki na mwenyekiti wa wasanii wa injili nchini Kenya Ringtone Apoko ametathmini kwa muda picha ya pamoja ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta, rais mpya William Ruto na wake zao huko ikulu ya Nairobi na kupitia kwa hiyo picha, msanii Ringtone ametoka na ushauri kwa wanaume ambao bado hawajaingia kwenye ndoa na wanatarajia kuoa siku za mbeleni.

Msanii huyo mwenye utata kwa kuangalia picha hizo, aliona kwamba mama wa taifa aliyeondoka Margret Kenyatta pamoja na mama wa taifa wa sasa Rachael Ruto wote ni wafupi kuliko waume zao.

Hili likaja wazo la kutoa ushauri kwa wanaume ambapo Apoko aliwasihi wanaume siku zote na muda wote kuhakikisha wanaoa wanawake ambao ni wafupi kuwaliko.

Kulingana na Apoko, mwanaume ukitaka kufanikiwa katika maisha yako basi nyota yako ya bahati ipo katika kuingia kwenye ndoa na mwanamke uliyemzidi urefu.

Ringtone alizidi kutoa sababu zake za kushauri hivyo na kusema kwamba wanawake warfu wataiba nyota ya mafanikio yako na siku zote utabaki kuwa maskini mla jalalani.

“Tafadhali wanaume wote hakikisha mnaoa wanawake wafupi kaam mnataka kufanikiwa katika maisha yenu. Wanawake warefu kuwaliko wataiba nyota ya mafanikio yenu,” Ringtone aliandika kwenye Instagram yake kwa kizungu chake kibovu.

Mchekeshaji MCA Tricky alifurahishwa na ushauri huo na kuonekana kumuunga Ringtone mkono kwa kile aliongezea kwamba sababu nyingine wanaume wanafaa kufuata ushauri huo ni kwa sababu maisha yenyewe ni mafupi.

“Sababu nyingine ya kuoa mwanamke mfupi ni kwa sababu maisha yenyewe ni mafupi,” MCA Tricky aliandika kwa utani akimalizia na emoji ya kucheka.