Mluhya awatumia meseji Sauti Sol akiwataka kufanya remix ya VAIDA "Wazee wamenituma"

Kukosa kufanya hivyo kutatupelekea sisi kula huyo jogoo kwenye nembo yenu - Masika aliwatahadharisha.

Muhtasari

• Hili si ombi bali ni amri kutoka kwa jamii ya Abaluhya - Masika.

Job Masika alisema alitumwa na wazee kuwaambia Sauti Sol kufanya remix ya VAIDA
Job Masika alisema alitumwa na wazee kuwaambia Sauti Sol kufanya remix ya VAIDA
Image: Instagram, Facebook

Mwanume mmoja kwa jina Job Masika kwenye mtandao wa Facebook amepakia picha za meseji alizowatumia wasanii wa kundi la Sauti Sol akiwataka kufanya remix ya ngoma inayotamba kwa sasa hivi ya Kiluhya kwa jina Vaida, yake msanii Harry Richie.

 

Katika meseji hiyo, Masika ambaye katika mwisho wa meseji hizo alijiita kama mkuu wa jamii ya Bukusu aliwaandikia kiongozi wa bendi hiyo Bien Aime Barasa pamoja pia na msanii shoga Chimano akiwataka kuharakisha kufanya remix hiyo katika kile alisema kwamba ni wazee wa jamii ya Abaluhya ilimpa maagizo hayo ayafikishe kwa Sauti Sol.

“Nimeitwa na wazee wa jamii ya Abaluhya na nikaambiwa niwafikishie ujumbe kwamba tunataka remix ya VAIDA ikiwashirikisha haraka iwezekanavyo. Kukosa kufanya hivyo kutawazukia na athari kubwa sana, kwa mfano mkikataa kutii amri wewe utamea nywele kichwani mwako pamoja na sehemu zingine,” Masika alimuandikia Bien.

Vile Vile Chimano naye alirushiwa ujumbe wa kwake, maudhui yakiwa yale ya kutaka kundi la Sauti Sol kutimba studioni na kumtafuta Harry Richie kufanya remix hiyo.

“Salamu Chimano, natumai uko salama, nimetumwa na wazee wa jamii ya Abaluhya kuwataarifu kwamba tunahitaji remix ya VAIDA ikiwashirikisha. Hili si ombi bali ni amri kutoka kwa jamii ya Abaluhya. Kukosa kufanya hivyo kutatupelekea sisi kula huyo jogoo kwenye nembo yenu. Ushirikiano wenu utakubaliwa sana,” Masika alimtaka Chimano.