"Wanadada wenzangu nitawaonea!" Zuchu ataka kushindanishwa na kina Diamond, Harmonize, Kiba

Amedai kuwa ligi yake ni ya wanaume na kutaka kushindanishwa nao tu kuendelea.

Muhtasari

•Zuchu alijigamba kuwa hata anaweza kumwandikia wimbo msanii wa kiume ya kusiwe na yeyote atakayegundua.

•Aliwashukuru wazazi wake, Bi Khadija Kopa na Bw Othman Soud  kwa kuwezesha na kukuza  kipaji chake cha usanii.

Zuchu
Image: HISANI

Staa wa Bongo Zuhura Othman almaarufu Zuchu amejipiga kifua kuhusu ubabe wake katika utunzi na uimbaji wa muziki.

Zuchu ambaye kwa sasa anaaminika kuwa miongoni kwa wasanii bora wa kike nchini Tanzania na katika ukanda wa Afrika Mashariki sasa ametoa ombi kutoshindanishwa tena na wasanii wenzake wa kike.

Binti huyo wa Malkia wa Mipasho Khadija Kopa amedai kuwa ligi yake ni ya wanaume na kutaka kushindanishwa nao tu kuendelea.

“Kwa uandishi wangu yafaa kuwekwa kwenye ligi za wanaume, wadada wenzangu nitawaonea tu kwa heshima!” alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Malkia huyo kutoka Zanzibar alijigamba kuwa hata anaweza kumwandikia wimbo msanii wa kiume ya kusiwe na yeyote atakayegundua.

“Naachilia ngoma mbili mwezi huu,” alitangaza.

Aidha aliwashukuru wazazi wake, Bi Khadija Kopa na Bw Othman Soud  kwa kuwezesha na kukuza  kipaji chake cha usanii.

Zuchu amezaliwa katika familia ya usanii. Mama yake, Bi Kopa, ni msanii mkongwe wa taarabu anayetambulika sana Bongo.

Kaka zake wakubwa Suma Kopa na Black Kopa ni wasanii  tajika katika tasnia ya muziki nchini Tanzania. Ndugu yake marehemu Omar Kopa ambaye aliaga mwaka wa 2007 pia alikuwa mwimbaji maarufu wa taarab.

Zuchi alisajiliwa na Diamond kwenye lebo yake mwakani 2020 na umaarufu wake umeendelea kukua kila uchao. Alikuwa msanii wa pili wa kike kujiunga na  lebo ya WCB  baada ya Queen Darleen (dadake Diamond) ambaye alisainiwa mwaka wa 2016.