Usimdharau mtu kwa sababu ya maumbile yake, Nimepitia matusi mengi - Stevo Simple Boy

Msanii huyo alielezea kwamba hata mpenzi wake wa awali alimuacha kwa sababu ya upungufu huo

Muhtasari

• Nimepitia matusi na kuambiwa siwezi mpaka na wasanii wakubwa. Na hata nikaachwa na mpenzi sababu ya upungufu - Simple Boy.

Msanii Stevo Simple amezungumzia kwa hisia kali himizo la wimbo wake mpya
Msanii Stevo Simple amezungumzia kwa hisia kali himizo la wimbo wake mpya
Image: instagram

Msanii Stevo Simple Boy mwishoni mwa wiki jana aliachia wimbo wa harusi ambao alisema ndio mwanzo mkoko unaalika maua kuelekea arusi yake na mchumba wake mpya, Gee.

Katika wimbo huo, msanii huyo mweney weledi mkali wa kutema misemo na nahau za Kiswahili anamsifia mchumba wake kwa kukubali penzi lake.

Stevo alienda kweney ukurasa wake wa Instagram na kuachia maelezo marefu kuhusu himizo la wimbo wake na pia kuwapa watu funzo linalotokana na wimbo huo kwa jina Wedding Day.

Simple Boy aligusia kwamba kipindi akiwa chipukizi watu walikuwa wanamkejeli kutokana ma maumbile yake. Hadi wengine walianza kuunda vichekesho almaarufu memes kutokana na muonekano wake pindi tu alipopata upenyo katika tasnia kwa wimbo wa Mihadarati.

 Akielezea dhima ya wimbo wake mpya, Stevo alisema funzo kubwa ni kwamba usiwahi mdharau mtu kwa jinsi alivyo kwani  muumbaji ni Mungu pekee.

“Nyimbo yangu Wedding Day ina funzo kwamba usimdharau mtu kwa maumbile yake wala kumbeza kwa upungufu wake. Mungu yu na sababu ya kukuumba jinsi ulivyo, uwe mwanadada au mwanaume,” Simple Boy alieleza kwa hisia.

Alizidi mbele kuibua kumbukumbu za uchungu jinsi amepitia mengi katika karakana ya matusi ya kila aina na kila rangi kutokana na muonekano wake. Alizidi kusema kwamba hata mpenzi wake alimuacha kwa sababu ya upungufu wake.

“Nimepitia matusi na kuambiwa siwezi mpaka na wasanii wakubwa. Na hata nikaachwa na mpenzi sababu ya upungufu. Usikate tamaa, tia moyo na kuamini Mwenyezi Mungu wakati ukifika utatimiza ndoto na utapata wanaokupenda jinsi ulivyo. Usiogope hata kidogo, nina Imani kwamba nami siku moja nitafanya kitu kikubwa cha kuheshimika. Wewe ni mrembo hivyo tu jinsi ulivyo,” Stevo Simple Boy alimaliza kwa ushauri na himizo lililokwenda skuli na kuhitimu kwa pointi za daraja la kwanza.