Karen Nyamu afurahia kupokezwa keki na mfuasi wake

Seneta huyo maalumu alipokezwa keki hiyo na mfuasi wake kwa kufana katika kampeni mpaka kuzawidiwa wadhfa wa seneta maalumu.

Muhtasari

• Nyamu alikuwa na lengo la kuwania useneta kwa tikiti ya chama cha UDA ila baada ya mazungumzo, akakubali kumuunga mkono Askofu Margret Wanjiru.

Karen Nyamu apokea zawadi ya Keki kutoka kwa shabiki
Karen Nyamu apokea zawadi ya Keki kutoka kwa shabiki
Image: instagram

Seneta maalumu Karen Nyamu amefurahishwa baada ya mfanyibiashara mmoja kutoka soko tambarare la Gikomba kumnunulia keki za kumpongeza kwa uteuzi wake.

Nyamu alipakia picha ya keki hiyo kwenye Instagram yake huku akidhihirisha furaha yake kwa kitendo cha mfanyibiashara huyo wa kike aliyemtambua kama mwanamke shupavu.

Seneta huyo alimtambua mfanyibiashara huyo kwa jina Grace na kusema alikuwa mmoja kati ya watu waliokuwa mstari wa mbele kwenye soko la Gikomba kupigia kampeni na kunadi sera za chama cha rais William Ruto, UDA.

“Madam Grace, rafiki yangu ambaye alikuwa mstari wa mbele kujitolea kutupigia kampeni katika soko la Gikomba leo alasiri alinishtukizia na keki ya kunihongera kama zawadi. Haki tu vile mnanipenda,” Nuamu aliandika kwenye Instagram kwa furaha tele.

Seneta huyo ambaye anajiongeza kama wakili wa mahakama kuu alipendekezwa kwenye seneti na chama tawala cha UDA baada ya awali kukubali kutia kibindoni azma yake ya kuwania useneta Nairobi.

Nyamu alikuwa na lengo la kuwania useneta kwa tikiti ya chama cha UDA ila baada ya mazungumzo ya kina, aliraiwa kuiweka pembeni na badala yake kumuunga mkono Askofu Margret Wanjiru amabye aliibuka wa pili nyuma ya Edwin Sifuna wa ODM.