Harmonize na Kajala wafunga ndoa kwenye video mpya ya 'Nitaubeba'

Nilifanya hii kwa ajili ya mtu nimpendaye - Harmonize.

Muhtasari

• Jua kwamba kila neno kama sio herufi katika huu wimbo linaelezea kiasi gani mimi nakupenda - Harmonize alimuandikia Kajala

Msanii Harmonize usiku wa kuamkia leo Alhamisi ameachilia video ya wimbo wake mpya kabisa ‘Nitaubeba’ ambao katika video ile mchumba wake Fridah Kajala Masanja ndiye amecheza kama vixen.

Wimbo huo aliutoa jikoni wiki moja iliyopita ukiwa bila video na kwa kweli umeshabikiwa na wengi, mapokezi yakawa ya aina yake kutokana na weledi wake aliouweka katika mishororo na beti, lakini pia midundo ni ya aina yake.

Ujumbe mkubwa katika wimbo huo ni asilimia mia kwa mia amejitoa kwa mpenzi wake Kajala na hilo pia kando na maneno linaweza likaonekana kwenye video kwa njia ya vitendo.

Harmonize na Kajala kwenye video hii ambayo ndio inatesa kabisa mitandaoni hivi sasa ameashiria jinsi harusi yao itakavyokuwa, haswa ikizingatiwa kwamba baada ya kuvishana pete za uchumba miezi michache iliyopita, wengi wanasubiria harusi yenyewe kwa hamu isiyomithilika.

Baada ya kuachilia video hiyo, Msanii Harmonize alikimbia kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuachia ujumbe maridhawa akidokeza kwamba huo tu ndio mwanzo mkoko kualika maua.

Alisema video hiyo ni ‘dedication’ tosha kwa mpenzi wake Kajala na aliifanya kwa njia ya kipekee kwa ajili yake – maneno ambayo ukisikiliza ngoma yenyewe utakubaliana nayo moja kwa moja bila kuhitaji uchambuzi wa kina.

“Nilifanya hii kwa ajili ya mtu nimpendaye. Ni wakati wako sasa pia kumuimbia unayempenda. Hebu tafakari jinsi hiyo siku yetu itakavyokuwa, siku yetu muhimu. Ahsante sana meneja wangu mkubwa mke wangu Fridah Kajala kwa kusababisha hili litokee,” Harmonize alimsifia mpenzi wake ambaye pia ni meneja wa kazi zake za muziki.

 Pia alifunguka kuwa kila neno na kila tukio katika wimbo huo pamoja pia na video yake ni ishara tu ya kila kitakachotokea katika siku ya ndovu kumla mwanawe, siku ya kufunga pingu za maisha ambayo wangali bado kuiweka wazi.

“Jua kwamba kila neno kama sio herufi katika huu wimbo linaelezea kiasi gani mimi nakupenda. Inshallah Mungu atuongoze pamoja na wapendanao wote. Tufike hiyo siku,” Harmonize aliongeza.