Harmonize atangaza kuondoka kwa baadhi ya wasanii Konde Gang tarehe 10 Octoba

Alisema hiyo ndio itakuwa siku ya kuadhimisha miaka 4 tangu kuanzishwa kwa lebo ya wasanii kadhaa watahitimu

Muhtasari

• Lengo ni kujikwamua kama watoto wa kimaskini. Tunatarajia kufanya jambo kubwa katika siku hiyo - Harmonize.

Harmonize natangaza kuondoka kwa baadhi ya wasanii Konde Gang mwezi kesho
Harmonize natangaza kuondoka kwa baadhi ya wasanii Konde Gang mwezi kesho
Image: instagram

Msanii Harmonize ambaye ni bosi wa lebo ya Konde Music Worldwide ametangaza kwamba huenda mwezi ujao wa Octoba wasanii kadhaa wakaoneshwa mlango na kuondoka lebo hiyo.

Harmonize alidokeza haya Alhamis kupitia instastory yake ambapo alisema kwamba mwezi ujao lebo ya Konde itakuwa inatimiza miaka 4 tangu aizindue alipoondoka Wasafi ya Diamond Platnumz.

Ujumbe huo wa Harmonize kuwa baadhi ya washirika wataondoka kwenye lebo ya Konde umepokelewa kwa njia tofauti tofauti huku macho ya wengi sasa yakiwa ni kwa wasanii Anjella na Killy na Ibraah ambao ndio wasanii wenye mikataba yao bado Konde.

Itakumbukwa mwaka jana msanii Country Boy alikatisha mkataba wake na kuondoka zake huku pia msanii mkongwe H-Baba mapema mwaka huu akiondoka huko, wala haikuwa imewekwa wazi ikiwa yeye alikuwa na mkataba na Konde Gang.

Katika ujumbe huo, Harmonize alisema hafla mwezi Octoba utakuwa mkubwa na wenye mishe nyingi kwa lebo hiyo kwani ndio watapiga tafrija ya kufikisha miaka minne pamoja pia na baadhi ya washirika wao kung’atuka.

“Tarehe 10 mwezi Octoba hapa Konde Gang tutatimiza miaka minne, sio rahisi asikuambie mtu. Vipidni vya kucheka, kulia, kuteleza na kuamka, yote kwa yote tunamshukuru Mungu pamoja na wewe unayesoma umefanikisha kuifanya Konde Gang kuwa lebo kubwa Afrika Mashariki. Ahsante sana,” Harmonize aliandika.

Alisema kwamba lengo kubwa la kuianzisha lebo hiyo ni kujaribu kusaidia vijana wa kimaskini kujikwamua kimaisha.

“Lengo ni kujikwamua kama watoto wa kimaskini. Tunatarajia kufanya jambo kubwa katika siku hiyo. Kubwa kwetu ikiambatana na kuhitimu kwa baadhi ya members kadhaa wa Konde Music. Mkesha tarehe 9 mwezi wa kumi,” Harmonize aliandika.