Kusah: Ex wangu Ruby akinialika harusi yake nitaenda na kumwimbia 'I Wish'

'I Wish' ni wimbo maarufu kutoka kwa msanii Kusah ambao unafanya vizuri sana kwenye mitandao ya kijamii

Muhtasari

• Kusah alisema Ruby akimpa mwaliko kwenda katika harusi yake atakubali na kumwimbia wimbo wake maarufu I Wish.

• Msanii huyo alisema Ruby akiolewa atafurahi sana kwa sababu itakuwa njia moja ya mwanawe kupata maisha mazuri.

Kusah akubali kuenda kwenye harusi ya aliyekuwa mpenzi wake Ruby
Kusah akubali kuenda kwenye harusi ya aliyekuwa mpenzi wake Ruby
Image: instagram

Wikendi iliyopita msanii Ruby alizua gumzo mitandaoni baada ya kusema kuwa akibahatika kufanya harusi basi barua ya mwaliko katika harusi hiyo ya kwanza atamkabidhi aliyekuwa mpenzi wake kwa maana ya Ex.

Moja kwa moja wengi wanaofuatilia maisha yake walijua hapa alikuwa anamlenga msanii Kusah ambaye alikuwa mpenzi wake kabla ya kutengana kwa shari mno.

Kusah na Ruby walikuwa wapenzi ambapo pia walibarikiwa kuwa na mtoto mmoja na Kusah katika mahojiano kadhaa amekuwa akinukuliwa akisema kwamba Ruby alimfungia hawezi kumuona mwanawe hata kidogo.

Ruby pia alisema kuwa kwa sasa yupo katika mahusiano na mtu ambaye si msanii na akasema hayupo tayari kwa sasa kumtambulisha kwenye mitandao ya kijamii.

Alipoulizwa ni kwa nini hataki kumruhusu Kusah kumuona mtoto wao, Ruby alimsuta Kusah vikali kwa kusema kwamba msanii huyo hana lolote hata hela ya kuunga bando kwenye simu yake ni mtihani mkubwa, sembuse kumhudumia mtoto!

Kusah ambaye ni mkali wa kibao cha ‘I Wish’ katika mahojiano na Refresh ya Wasafi alizungumzia madai haya na kusema kwamba Ruby ana mume wake lakini bado anazidi kumfuatilia mpaka kujua kwamba ameweka rangi gani kwenye kichwa chake.

Msanii huyo ambaye wiki hii ameachia albamu yake mpya kwa jina ‘Romantic’ pia alizungumzia uwezekano wa kuhudhuria harusi ya Ruby na mumewe iwapo atapewa barua.

“Ndio harusi mimi nitakwenda, siwezi kata mwaliko, nitakwenda na nitamwimbia ‘I Wish’, nitafurahi sana kwa sababu itakuwa ni njia moja ya mwanangu kuishi maisha mazuri kwa sababu mwanamke ambaye siku zote yuko mzingatifu kwa mwanaume mmoja, amekaa naye maisha yanaendelea wanafanya mambo yao, ni mwanamke ambaye anajitambua. Kwa hiyo itamsaidia pia mwanangu kuwa na maisha mazuri kwa upande wake,” Kusah alisema.