Mwanamke aenda nyumbani kwa Amira bila idhini yake, aacha barua baada ya kumkosa

Amira alisema mwanamke huyu aliyeenda kwake bila kutarajiwa alitafuta namba yake ya simu kisha kumtumia ujumbe.

Muhtasari

•Mwanadada huyo anayeitwa Daisy alimuomba Amira msamaha kwa kuenda nyumbani kwake bila idhini yake ila Amira hakuichukulia vizuri bado.

Amira
Image: Being Amira Instagram

Aliyekuwa mke wa kwanza wa mfanyibiashara Jimal Rohosafi, Amira amfokea mama aliyeenda na kuingia nyumbani kwake bila idhini yake.

Amira alisema mwanamke huyo aliyetembeleaa nyumba yake wakati hakuwa nyumbani. Aliwaambia walinda lango kuwa yeye ni rafiki yake.

Aliongeza na kusema mwanamke huyo alipoambiwa kuwa Amira hayuko nyumbani bado aliingia sebuleni mwa nyumba hiyo, kisha akaketi kitako kwenye sofaseti  ya Amira na kusema kuwa hataondoka ila atamsubiria Amira arudi nyumbani.

"Huo ni ujasiri mkubwa!Yaani anaona ana haki kama hiyo?" alisema Amira aliyekuwa amejawa na hasira.

Alisema aliyekuwa nyumbani aliwasiliana naye na kumwambia kuwa ana mgeni kisha kumuuliza mgeni huyo aandaliwe maankuli yepi. Amira alisema alimwambia mfanyikazi wake kuwa hakuwa anatarajia mtu yeyote.

Baada ya kisa hicho Amira alisema mwanamke huyu aliyeenda kwake bila kutarajiwa alitafuta nambari yake ya simu kisha kumtumia ujumbe.

Mwanadada huyo anayeitwa Daisy alimuomba Amira msamaha kwa kuenda nyumbani kwake bila idhini yake ila Amira bado hakuichukulia vizuri.

"Nakuomba msamaha kwa kuenda nyumbani kwako bila idhini yako, haikuwa kwa kutaka na naelewa haswa ni kwa nini umekasirika hivi. Ninakuahidi ya kwamba nitaiheshimu idhini yako na faragha huko mbeleni. Natumai utanisamehe," Daisy alisema.

Daisy alimwambia Amira kuwa alielewa alivyohisi baada yake kufanya kitendo hicho na kuwa angependa kurekebisha makosa yake na angefanya chochote ili Amira aweze kumsamehea.

Alisema pia alikuwa amemwachia Amira bahasha na ujumbe wake kwenye ofisi yake na angetaka Amira amjulie wakati mwengine.

Amira bado hakufurahia kitendo alichofanya Daisy.

"Na bado anaenda kutafuta nambari yangu ya simu ili aombe msamaha!" alifoka.

Amira alisema kuwa kujua mahali anapoishi mtu si sababu ya kuenda kwake bila ujumbe au idhini yake na kuwa watu wazoee kuheshimu faragha za nyumba za watu.