Joy Kawira: Kuna siku mume wangu alinifuata hadi kazini na kunipiga, ni mchungaji wa kanisa

Kawira alisema kipindi hicho akifanya kwa redio mumewe alimfuata na kumpiga na baadae akarudi na kuendelea kazi hewani.

Muhtasari

• Muigizaji huyo alieleza kuwa hangeweza kumripoti mumewe popote kutokana na kwamba mumewe alikuwa anampiga sehemu za mwili zisizoweza kuonesha ushahidi wa kupigwa.

Joy Kawira afunguka jinsi alivyopitia ndoa yenye mateso na mchungaji
Joy Kawira afunguka jinsi alivyopitia ndoa yenye mateso na mchungaji
Image: Instagram

Aliyekuwa muigizaji wa Papa Shirandula, Joy Kawira amezungumzia jinsi alivyopitia dhuluma katika ndoa yake.

Kawira ambaye alikuwa mtangazaji katika kituo kimoja cha redio humu nchini alikuwa anazungumza na mtangazaji wa Radio Jambo Massawe Japanni jinsi alipitia makuruhu mengi kwenye ndoa yake iliyovunjika.

Muigizaji huyo wa Vioja Mahakamani alieleza kuwa kuna siku aliyekuwa mume wake alimfuata mpaka kazini katika kituo cha redio na kumpiga makofi na mateke.

Kawira ambaye wakati huo alikuwa anafanya kipindi cha usiku katika redio, mumewe alimfuata usiku huo hadi katika ofisi za redio hiyo na kumpa kipigo cha mbwa msikitini kwa kile alikuwa anamuuliza ni kwa nini hakurejea nyumbani.

Muigizaji huyo alieleza kuwa aliyekuwa mumewe baada ya kumpiga usiku, ambapo hata mlinzi wa usiku aliyekuwa hapo hakuweza kumsaidia, alijikusanya na kurudi studioni na kuendelea na kipindi.

"Nilikuwa nimeenda kwa mama yangu, lakini nilimwambia niko kazini. Alinipiga tukiwa kwenye lifti za ofisi. Kulikuwa na mlinzi pale lakini hakufanya chochote," Kawira alisema.

Baadae alipomaliza kipindi aliondoka na kuenda kulala kwingine kwa kuogopa kurudi nyumbani kwa mumewe.

Kawira ambaye ndoa yake ilivunjika mwaka jana baada ya kudumu kwenye ndoa kwa miaka 6 alisema kwamba aliyekuwa mumewe huyo alikuwa anampiga vipigo baada ya vipigo.

Akizungumza ni kwa nini hakuweza kumripoti katika vyombo vya sharia hata mara moja, Kawira alisema hakuona haja kwa sababu mumewe alikuwa anampiga sehemu ya mwili ambayo haingeweza kuonesha dhibitisho kuwa kweli amepigwa.

"Ni mtu mwerevu, alikuwa ananipiga mahali hutabaki na ushahidi. Ulimi wake ni mtamu, ata ungesema mimi ndiye mwenye makosa," alimwambia Massawe.

Vile vile alieleza Massawe kuwa mumewe ni mtu mwenye mdomo wa kumtoa nyoka pangoni kwani angemfanyia mambo mabaya na ikifika kwa watu anajitetea mpaka Kawira anaonekana tena ndiye mwenye makossa ya kumsingizia tu mumewe.

Mumewe huyo walikutana kanisani na kilichoshangaza wengi ni kwamba mumewe huyo ni mchungaji wa kanisa tajika sana.

“Watu wachache ambao nilizungumza nao kanisani walikuwa wananiambia kwamba mwanamke ni kuvumilia, na siku zilizidi kupita mateso yakizikaripia,” Kawira alieleza Massawe Japanni katika kipindi cha Ilikuaje.

Alisema mambo mengine mengi hangetaka kuyazungumzia sana kwa sababu tu ya kulinda heshima ya watoto wake.

Muigizaji huyo aidha alipuuzilia mbali dhana au hata fikira ya kurudi katika ndoa tena katika siku zake za usoni kwa kile alisema kuwa moyo wake katika mapenzi ulikufa kabisa kutokana na mumewe ambaye ni mhubiri kumpa kipigo sana.

Kawira alisema kuwa kama kuna kitu kikubwa ambacho anakijutia kabisa katika maisha yake ni ile siku aliyokwenda kwenye hafla ambayo alimkuta mchungaji huyo ambaye baadae alikuja kuwa mumewe wa kumtesa vibaya.