Msanii namba moja kwa miziki ya kizazi kipya nchini Kenya, Otile Brown amekuwa mtu maarufu wa hivi punde kurusha dongo kwa mwanasosholaiti mstaafu Vera Sidika baada ya kupakia picha mpya akiwa amepunguza makalio.
Jumatano, Vera Sidika aliweka wazi kupitia picha pamoja pia na maelezo marefu kuwa aliamua kuchukua uamuzi huo mgumu wa kupunguza shepu yake ya maungo kutokana na sababu za kiafya.
Sidika alisema kuwa upasuaji aliofanyiwa kuongeza makalio ulikuwa umeanza kumtafuta mpaka kulazimisha kufanyiwa upasuaji mwingine wa kupunguza makali mpaka shepu hiyo mpya aliyoonekana nayo na ambayo sasa imemgeuza kichekesho katika mitandao ya kijamii.
Wengi wanaofuatilia Sanaa ya Kenya wanajua kuwa miaka kadhaa nyuma msanii Otile Brown walikuwa katika mahusiano ya kimapenzi na Vera Sidika, mahusiano ambayo hayakudumu kwa muda mrefu.
Sidika alimbwaga Otile Brown kwa kile wadaku walisema ni kutoridhika na jinsi Brown alikuwa anamdekeza katika sinia la mapenzi.
Otile Brown sasa ameibuka na ujumbe fiche kupitia instastory yake ambao unaonekana kumlenga moja kwa moja Vera Sidika kuhusu umbo lake la awali ambalo sasa imebainika lilikuwa la bandia.
“Ilmradi mimi ninajua kuwa nilidumisha kuwa mkweli na asilia bila kuwa bandia kwa njia yoyote kutoka upande wangu, niko vizuri na jinsi mambo yanavyozidi kuchanua,” Otile Brown alirusha bomu la moto kwenye makalio ya Sidika.
Sidika alikuwa mwanadada mwenye umbo la kutamanisha kila mwanaume ambaye alikuwa anampita, lazima angegeuka mara mbili mbili nyuma kusifia ‘kazi ya Mungu’ katika mwili wa Sidika – pasi na kujua kuwa ilikuwa bidii ya upasuaji baada ya upasuaji.