logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Ugali Man azungumzia maisha yake ya uchochole kabla ya bahati kubisha hodi

Odibet ilimpa dili ya kima cha shilingi milioni  5.

image
na Radio Jambo

Habari18 October 2022 - 09:24

Muhtasari


• Ugali man alisema kuwa bado hawezi kuelezea jinsi video yake ilivyoenea kwani madhumuni yake kurekodi video ilikuwa kwa ajili ya kujifurahisha.

Charles Odongo almaarufu kama 'Ugali man'

Charles Odongo almaarufu Ugali Man, si jina geni kwa masikio ya wakenya.  Ugali Man alipata umaarufu  sana mwaka wa  2021, baada ya wakenya kufurahishwa na Klipu yake alipokuwa akidaka ugali hewani huku akila mlima wa ugali.

Klipu hiyo haikumpa umaarufu tu mbali maisha yake yalibadilika kabisaa.

Akizungumza katika mahojiano kwenye Chaneli ya Youtube ya Mungai Eve, Ugali Man alisema kuwa amepitia mengi na aliteseka sana kabla ya kufika pale aliko sasa. Kwanza alisema ni neema kutoka kwa mwenyezi Mungu kwani alianzia maisha kwenye nyumba iliyodorora sana huko Kware.

Huko Kware maisha yake hayakuwa ya kuridhisha kwani aliishi kula mlo mmoja tu kwa siku na hata kulala njaa. Ila alikuwa mchapakazi kwenye maeneo ya ujenzi ili kukidhi mahitaji ya familia yake.

Hivi majuzi wakati Virusi vya Corona vilibisha nchini mambo yalianza kuwa mabaya zaidi alipopoteza kazi. Kutokana na hali ya uchochole alishindwa kulipa kodi ya nyumba na kufungiwa nje. 

Babake kutokana  na mapenzi yake alimpa kipande kidogo cha ardhi ajenge nyumba ya kuishi na familia yake.

Kwa kuwa hakuwa na kazi, aliamua kuanzisha eneo la gym nyumbani  na kutoza kati ya shilingi 20 hadi 50 kwa siku.

Lakini haikuwa kama kazi kwake bali ilikuwa tu kujifurahisha tu kwani haikumletea pesa za kutosha.

Baada ya dhiki ni faraja. Ugali man alisema kuwa bado hawezi kuelezea jinsi video yake ilivyoenea kwani madhumuni yake kurekodi video ilikuwa kwa ajili ya kujifurahisha.

Video hiyo ambapo alikuwa akifinyanza tonge la ugali kulirusha juu na kulidaka kwa madaha ilisambaa katika kurasa zote za mitandao ya kijamii na hapo ndipo umaarufu wake ulianza.

Sasa anafanya kazi na kampuni ya Odibet iliyompa  kandarasi nono na kumweka kuwa balozi wao.

Kwenye dili hiyo walimpa shilingi milioni  5, pesa ambazo zilimsaidia kugharamia biashara yake ya kunoa misuli huko Rongai na kununua gari la kubeba watalii.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved