Nini Wacera, mwigizaji mkongwe katika Sanaa ya filamu nchini Kenya amefunguka maisha yake ya ujana na maamuzi ambayo alifanya kipindi hicho ambayo yanazidi kumwandama mpaka leo hii.
Wacera alikiri kutoa mimba alipokuwa tineja, tukio ambalo alisema lilimuuma sana.
Wacera ambaye ni mama wa miaka 44 alikuwa anazungumza na jarida la Parents Magazine, baada ya kurejea kwenye runinga tena ambapo aliigiza katika filamu ambayo inaoneshwa kwenye mtandao wa Netflix, Country Queen.
Mwigizaji huyo alisema kwamba alipata ujauzito akiwa na miaka 19 tu ambapo alilazimika kutafuta suluhu ya kuutokomeza, suluhu lenyewe likawa ni kuharibu mimba ile.
Alikuwa akizungumzia ajenda kuu ya mwezi huu wa Oktoba ambayo inalenga kuwahamasisha wanawake waliopoteza ujauzito na kusema kwamba alichukua uamuzi huo kwa sababu hakuwa na mtu wa kumsapoti.
“Ninahisi kama ni tukio moja katika maisha yangu ambalo lilinipasua hadi kiini cha roho yangu kwa sababu ilikuwa ya kiwewe. Utoaji mimba huo ulichukua kama siku nzima. Baada ya yote, wewe ndiye msichana mlegevu ambaye ulishiriki kitendo na mpenzi wako na kupata mimba,” asema kwenye toleo la Oktoba.
Mwigizaji huyo mkongwe alisema kwamba hali hiyo ilimfanya hata kujiua - alijaribu kujiua lakini mama yake aliingilia kati. Hata hivyo, aisema hakupata ushauri unaohitajika.
Kutokana na uzoefu wake, Wacera anaamini tamaduni za Kenya ambapo elimu ya kushiriki mapenzi inaendelea kuchukuliwa kuwa mwiko inahitaji kufutiliwa mbali.
"Uchanya wa kushiriki kitendo hufundisha watu jinsi ya kuthamini mapenzi na mawazo chanya. Pia ni kibali cha kufundisha. Niliponyanyaswa kingono nilipokuwa mtoto, sikuweza kumwambia mama yangu kuhusu hilo kwa sababu ngono haikuzungumziwa hadharani,” alinukuliwa kwenye jarida hilo.
Alipata umaarufu mwaka wa 2005 alipokuwa miongoni mwa waigizaji wakuu wa Wingu La Moto, kipindi cha Soap Opera kilichoonyeshwa kwenye runinga ya NTV kwa miaka mitatu.