Akon ni jina maarufu sana katika Sanaa ya muziki si tu Marekani bali duniani kote. Huyu ni msanii Mmarekani mweusi ambaye ana mizizi yake kutoka taifa la Senegal.
Kando na muziki wake na jina lake la Sanaa – Akon, wengi hawajui jina lake halisi huku wengi wakiamini hilo ndilo jina linalopatikana hata kwenye stakabadhi zake.
Msanii huyo katika klipu ya video ambayo imesambazwa mitandaoni kwa mara ya kwanza ameweka wazi jina lake na kuelezea chimbuko halisi ya jina hilo.
Kilichowachekesha wengi, jina la msanii huyo ni refu kiasi kwamab mtu akilitamka utadhani ni kukariri mshororo wa shairi ambao vina vyake vimeoanishwa kwa njia stadi ya ushairi.
Katika klipu hiyo ambayo alikuwa anafanya mahojiano ya kipekee na mtangazaji mmoja wa redio aliyetaka kujua jina lake kwa ukamilifu, msanii Akon alitamka kama mtu ambaye anaimba, kitu ambacho kilimshtua mtangazaji huyo na kumtaka kulitamka kwa mwendo taratibu na kuelezea pia.
“Aliaune Damalla Bouga Time Puru Nacka Lu Lu Lu Bandara Akon Thaim” msanii huyo alijibu kuwa huo ndio urefu wa jina lake.
Alieleza kwamba katika jamii ambako anatoka, mtoto wa kiume wa pili kutoka kwa mtoto mkubwa wa familia huwa anapatiwa jina na kila mtu katika ukoo.
Jina hili lake refu liliwaacha wanamitandao walioona video hiyo wakizua vichekesho na utani huku wengine wakisema kwamba jina lake ni kama kukariri punji za tasbihi.