Staa mpya kabisa kweney tasnia ya muziki wa Bongo Fleva, Jay Melody kwa mara ya kwanza kabisa ameonesha picha ya mpenzi wake wakiwa wanajivinjari katika mbuga ya wanyama.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Jay Melody alipakia vipande vya video akionekana kufurahia uwepo wa mpenzi huyo wake huku wakiwa karibu na mbuni na nyingine wakiwa wanawalisha pundamilia kwa tabasamu kubwa.
Melody hakusita kudhihirisha upendo wake kwa mpenzi wake na aliandika maneno kwamba anampenzi, huku wimbo wake ambao unazidi kufanya vizuri kwenye majukwaa ya kupakuwa miziki ‘ Nakupenda’ ukiwa unacheza na kukamilisha taswira na mandhari ya mahabuba hao.
"Siku tumeifurahia vizuri, nampenda jamani," Melody aliandika.
Kwa muda mrefu msanii huyo alikuwa hajawahi kuonekana hadharani na mpenzi wake huku akiibua gumzo pevu mitandaoni miezi michache iliyopita baada ya kupakia picha yake pamoja na ya mjasiriamali mdogo, Paula Kajala.
Katika chapisho hilo ambalo alilazimika kulifuta kutoka kwenye Instagram yake, Melody alikuwa amepakia picha yake zikiwa zimeangaliana na ya Paula huku akiachia maelezo mafupi yanayoashiria mahaba, jambo ambalo liliwafanya watu kuzungumza huku wakikisia kuwa huenda wawili hao wako kwenye mapenzi.
Hili lilitokea pindi tu baada ya Paula kuweka wazi kwamba hakuwa tena pamoja na msanii Rayvanny kimapenzi. Aliyaweka haya wazi wakati anafungua duka lake la nguo, Paula Closet.
Melody baadae pia kutokana na shinikizo la kutakiwa kunyoosha maelezo na mashabiki wake, alilazimika kuifuta picha ile na katika mahojiano na Refresh ya Wasafi alikana kuwa katika mapenzi na Paula.
Alisema kwamba yeye anamkubali tu kwa urembo wake na kupakia picha ile haikuwa na maana yoyote kwamba wanatoka kimapenzi.
“Kama utakuwa ulikuwepo makini sana utagundua kulikuwepo na picha mbili. Picha moja ni ya kwangu nimepiga na ua kichwani na ya pili ni ya Paula. Mimi nampenda kama miongoni mwa watu wengine ninavyowapenda. Namuona picha zake nzuri na ile niliyoipakia niliipenda lakini maelezo niliyofuatisha kwenye picha zile hayahusiani na picha yake,” Jay Melody aliitetea hatua yake ya kupakia picha ya Paula sambamba na yake.
“Sema tu nilivyoona yale maoni ya watu nikaona sina haja ya kumtengenezea mtoto wa watu msongo wa mawazo ndio maana nikaitoa maana pale walikuja hadi wajomba zake. Mimi naheshimu sana watu, hata Paula nampenda, namuona anapiga picha kali ndio maana nikaipakia tu,” Jay Melody aliongeza katika mahojiano hayo.