Wahu aelezea upendo wa bintiye wa pili kwa dadake mdogo

Nyakio alikuwa akiukumbatia ujauzito wa mamake kabla ya kujifungua

Muhtasari

• Nyakio amekuwa akimkumbatia Shiru kila usiku baada ya mama yake kujifungua.

Nyakio kabla na baada ya uja uzito

Mwanamuziki Wahu ni mwenye furaha kwa jinsi mabinti wake walivyopokea jukumu lao la kumsaidia kulea dada yao mdogo, Shiru.

Alilinganisha jinsi mtoto wake wa pili, Nyakio alikuwa akikumbatia mimba yake kabla ya kujifungua.

Alipakia video mbili katika Instastory zake kuonyesha jinsi binti yake alipenda kuwa na dada mdogo.

"Nyakio alikuwa anakumbatia ujauzito wangu kila usiku kabla ya kujifungua," Wahu aliandika kwenye video ya kwanza.

Aliweka wazi kuwa baada ya kujifungua, Nyakio amekuwa akijikaza kumlea mtoto wao mdogo na hata kulala naye kila usiku.

"Na sasa, huyu ni Nyakio kila usiku," alisema katika video iliyoonyesha Nyakio akilala na dada yake mdogo.

Nyakio alikuwa amemkumbatia Shiru kwenye usingizi, jambo lililoonyesha ukaribu wake na dada yake.

Hivi majuzi, mwanamuziki huyo alipakia picha ya Nyakio akiwa amelala na dada yake mdogo ambapo Wahu alisema alikuwa bafuni na alipotoka alikutana na tukio hilo la kuvutia.

Mabinti wa Wahu hawajasita kumpa mama yao cha kujivunia .

Jana Jumanne, Wahu alipakia picha ya bintiye Tumiso akimlea Shiru, jambo ambalo lilimfurahisha mwanamuziki huyo.

"Picha iliyo na hisia nyingi, mapenzi matamu," Wahu aliandika huku akimwashiria Tumiso kama mama mlezi mdogo.

Kabla ya Wahu kujifungua, mume wake Nameless alikuwa amemsifia Tumiso kwa kuwa binti bora na kujivunia kuwa baba yake.

Nameless alisema kuwa Tumiso alikuwa mfano bora tayari kwa Nyakio na aliamini kuwa ataendeleza hilo kwa Shiru.

Nyakio amekuwa akifuata nyayo za Tumiso za kumsaidia mama yao kumlea Shiru kwa njia ya kusisimua.