Vera Sidika: Nguo ya 'birthday' ya Asia inagharimu 30K, tuliagiza kutoka USA

Nguo ile tuliiagiza kutoka Florida, Marekani - Sidika.

Muhtasari

• Kupitia Instastories zake, Sidika alidokeza kuwa nguo hiyo haijanunuliwa nchini Kenya.

• Miezi kadhaa awali pia alinukuliwa akisema kitanda cha mwanawe alikiagiza kutoka Uingerea kwa thamani ya 300K

Sidika adokeza bei ya nguo ya mwanawe Asia Brown
Sidika adokeza bei ya nguo ya mwanawe Asia Brown
Image: Instagram

Mwanasosholaiti Vera Sidika amezidi kupandisha hadhi ya bintiye Asia Brown baada ya kufunguka kuhusu nguo yake ambayo alionekana nayo juzi wakati wa kusherehekea kufikisha mwaka mmoja tangu kuzaliwa.

Kupitia Instastories zake, Sidika alidokeza kuwa nguo hiyo haijanunuliwa nchini Kenya bali ni mali safi ambayo imeagizwa kutoka miji ya Wazungu kwa bei ghali kuzidi maelezo.

Sidika alisema kwamba nguo ya Asia Brown alioonekana nayo siku ya sherehe yake imekuwa ikiuliziwa na watu wengi kwenye DM yake na ndio maana aliamua kuweka paruwanja kila kitu kupitia ukurasa huo.

Kwa kuwashangaza wengi, Sidika alisema nguo hiyo iliagizwa kutoka jimbo la Florida nchini Marekani kwa takriban dola 250 ambazo ukibadilisha kwa madafu ya maskani Kenya ni elfu 30 na machenji juu.

“Wengi wenu mnaniuliza nguo ya sherehe ya siku ya kuzaliwa ya Asia Brown. Nguo ile tuliiagiza kutoka Florida, Marekani. Iliuzwa kwa takribani $250 (Ksh 30,337) na tuliinunua kutoka kwa muuzaji mmoja kwa jina Adaaziza. Nguo ya kipekee na yenye haiba ya aina yake kwa mtoto,” Vera Sidika alijipiga kifua.

Ikumbukwe hii si mara ya kwanza kwa mwanasosholaiti huyo ambaye pia juzi ameachia ngoma kumpaisha mwanawe kwa maisha ya kifahari.

Mapema mwaka huu, alidokeza kwamba kitanda cha watoto alichomnunulia Asia kiliagizwa kutoka nchini Uingereza kwa takribani elfu 300 pesa za benki kuu ya Kenya.