Hata nikifa leo, najua inavyohisi kuwa nambari moja- Harmonize ajigamba

Harmonize amejivunia mafanikio ya albamu yake mpya 'Made For Us.'

Muhtasari

•'Made For Us' imefanikiwa kupata streams zaidi ya milioni tatu kwenye mtandao wa Boom Play katika kipindi cha wiki mbili pekee.

•Mwimbaji huyo mahiri pia alijivunia albamu yake kuongoza nchini Tanzania kwenye mtandao wa Audio Mack.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amejivunia mafanikio ya albamu yake mpya 'Made For Us.'

Albamu hiyo ya tatu ya bosi huyo wa Konde Music Worldwide yenye nyimbo 14 imefanikiwa kupata streams zaidi ya milioni tatu kwenye mtandao wa Boom Play katika kipindi cha wiki mbili pekee.

Konde Boy amesherehekea mafanikio hayo makubwa na kubainisha kuwa yamemfanya apate hisia za ushindi.

"Hata nikifa leo, najua inavyohisi kuwa nambari moja kwenye mchezo," alisema kwenye Instastori zake.

Alijigamba kuwa hakuhitaji utangazaji wa vyombo vya habari, matangazo mengine yoyote wala machawa kufanikisha ushindi huo.

"Ni Mungu pekee na watu wazuri waliofanikisha," alisema.

Mwimbaji huyo mahiri pia alijivunia albamu yake kuongoza nchini Tanzania kwenye mtandao wa Audio Mack.

Harmonize aliachia albamu ya 'Made For Us' mwishoni mwa mwezi Oktoba, ikiwa albamu yake ya tatu kufikia sasa.

Nyimbo katika albamu hiyo ni pamoja na;- Mwenyewe, My Way, Leave me alone, Wote, Nitaubeba, Utanikumbuka, I miss you, Die, The way you are, Miss Bantu, Best Friend, Deka, Too Much na Amelowa.

Harmonize alitoa shukran za dhati kwa mchumba wake Frida Kajala kwa kumsaidia katika utayarishaji wa albamu hiyo.

"Umeifanya akili yangu iwe na utulivu, naweza tunga mistari inayostahili. Ulifanya kazi kubwa zaidi kuboresha albamu hii. Asante na nakupenda, mke wangu na boss wangu," alimwambia kwenye Instagram.

Aidha alidokeza kwamba albamu hiyo huenda ikawa ndio yake ya mwisho kufanya nyimbo kwa lugha ya Kiswahili.