Wakana Mungu waomba msaada wa pesa kulipa kodi ya afisi zao

Tunahitaji usaidizi wako ili kusaidia jamii yetu kulipa kodi ya kila mwezi ya KShs 18000/=, saidia jamii yetu - Atheists walisema.

Muhtasari

• Jamii hiyo awali ilikuwa imeonesha kufurahia kwao baada ya agizo la gavana wa Kisumu profesa Anyang’ Nyong’o kutaka maeneo ya kuabudu yanayopiga kelele kufungwa.

Rais wa Atheists Kenya, Harrison Mumia
Rais wa Atheists Kenya, Harrison Mumia
Image: Twitter

Jamii ya watu wasioamini Mungu nchini Kenya imeomba msaada wa pesa kwa Wakenya ili kusaidia kulipa kodi ya makao ya afisi zao ambazo zinakaribia kufungwa kwa kutolipa kodi.

Wakifichua hayo kwenye Twitter Jumatatu, Novemba 7, jamii hiyo ya watu wasioamini waliomba usaidizi wa kuchangisha KSh 18,000 ili kulipia kodi ya ofisi ya kila mwezi ya shirika lao.

 Pia, kwa ushirikiano na Shirika la Haki za Kibinadamu kwa Wakana Mungu, jamii inaendesha kampeni ya kuchangisha pesa inayolenga kusaidia mahitaji ya haraka ya rais wao, Harrison Mumia.

“Pesa hizo zitamsaidia rais, Harrison Mumia, kwa gharama za kukodisha akiwa kati ya kazi - baada ya kufutwa kazi na mwajiri wake kwa tweet - ili aweze kuzingatia jukumu lake muhimu kama rais wa shirika pekee lililosajiliwa lisiloamini kuwa kuna Mungu nchini Kenya,” ujumbe huo ulieleza.

Jamii hiyo awali ilikuwa imeonesha kufurahia kwao baada ya agizo la gavana wa Kisumu profesa Anyang’ Nyong’o kutaka maeneo ya kuabudu yanayopiga kelele kufungwa.

“Tunahitaji usaidizi wako ili kusaidia jamii yetu kulipa kodi ya kila mwezi ya KShs 18000/= (USD147). Saidia jamii yetu,” waliandika kwenye Twitter.

Kwa muda mrefu, kundi hilo limekuwa likipinga vikali mambo ya kanisa ambapo wamekuwa wakirushiana cheche na aliyekuwa waziri wa elimu profesa George Magoha ambaye alibaki na msimamo kuwa watu wasioamini Mungu hawana nafasi hata kidogo kuwa na usemi katika jamii.