Kwa nini mamake Zuchu, Khadija Kopa alitoza Ksh 200 tu kwa shoo yake ya Mombasa?

Ijumaa ya Novemba 4, Kopa alikuwa anatumbuiza kwenye klabu moja Mombasa ambapo kiingilio kilikuwa shilingi 200 tu za Kenya.

Muhtasari

• Wengi walishangaa ni kwa nini malkia huyo ambaye amejizolea umaarufu lakini pia na heshima kubwa angependa kudai kiasi cha shilingi 200 kama kiingili.

Khadija Kopa na binti yake Zuchu
Image: HISANI

Wiki moja iliyopita, malkia wa mipasho ya taarab kutoka Tanzania, Khadija Kopa alikuwa na tamasha katika jiji la Mombasa eneo la Bamburi.

Kuwa na shoo Kenya si jambo kubwa kwa sababu si mara ya kwanza kwa mkongwe huyo wa muziki kufanya hivyo, bali gumzo kubwa lilikuwa kiasi cha pesa alikuwa anaitisha kama kiingili kwa yeyote aliyetaka kumtizama akitumbuiza kama kawaida yake jukwaani.

Kopa alipakia bango kwenye ukurasa wake wa Instagram ambapo kiingilio katika shoo yake hiyo iliyofanyika Novemba 4 kilikuwa shilingi 200 tu pesa za Kenya.

Wengi walishangaa ni kwa nini malkia huyo ambaye amejizolea umaarufu lakini pia na heshima kubwa angependa kudai kiasi cha shilingi 200 kama kiingili.

Kuna minong’ono kwamba mwimbaji huyo anatoza kiasi cha chini kwa maonyesho yake huku akipanga kuachana na miaka yake ya muda mrefu katika tasnia ya muziki.

Itakumbukwa katika mahojiano mwaka jana, mwimbaji huyo alifichua kwamba hivi karibuni anatazamia kustaafu na kuwaachia watoto wake urithi wake wa kimuziki ili waendelee nao.

Kopa amekubuhu katika tasnia ya muziki ambapo alianza safari yake ya kutumbuiza kwa mipasho mwaka 1990 na kundi lake la Cultural Music Club.

Binti yake Zuhura Othman Soud, anayefahamika kwa jina la kisanii Zuchu, amefuata sana nyayo zake za muziki akiwa mwimbaji. Zuchu alijiunga na Wasafi Records na kuachia ngoma ambazo zimemheshimisha katika Sanaa ya Bongo Fleva.

Khadija Kopa kwa mara kadhaa amesikika akijisifia urithi mkubwa wa kipaji alichokiacha kwa bintiye Zuchu na alisema kwamba sasa anaweza akastaafu kwa furaha na Amani kwani mwanawe Zuchu amemheshimisha.

Alisema kuwa pale kwa Zuchu bila shaka alipiga kite kweli na kuzaa toto la mafanikio kinyume na watu wengine wanaozaa watoto wasiowasaidia – kitu ambacho alikiita mtoto asiyekusaidia huyo si wa kumzaa bali wa kumnya.