Msanii wa 'Firirinda' Dick Njoroge aomba msaada wa kifedha

Kajei alifichua kuwa familia ya mwanamuziki huyo imepanga kuchangisha pesa ili kujaribu kukusanya kiasi kinachohitajika hospitalini.

Muhtasari
  • Firirinda ni wimbo wa kitamaduni unaoonyesha uchangamfu na furaha ya kuwakaribisha wageni

Mwanamuziki maarufu wa Mugithi Dick Njoroge Munyonyi ambaye alivuma sana mwaka wa 2021 baada ya kibao chake cha Firirinda anaomba msaada wa kifedha.

Mwanamuziki huyo anadaiwa kusumbuliwa na ugonjwa wa kifua kikuu ambao inasemekana aliupata miaka mingi baada ya kutoa wimbo wa ‘Firirinda’.

Akitoa ujumbe huo,mmoja wa wanamuziki kutoka kanda ya kati aliyetambulika kwa jina la Kajei Salim alisema alipokea simu kutoka kwa gwiji huyo, Dick Njoroge akisema amekuwa mgonjwa na anahitaji msaada wa kifedha ili kugharamia bili yake ya matibabu zaidi ya Sh milioni 1.5.

"Wapenzi, wasanii na mashabiki wa Dick Njoroge Munyonyi 'Firirinda'. Ninaandika chapisho hili kuhusiana na simu niliyopokea kutoka kwa gwiji wetu Dick Munyonyi

Alinifikia na kuniambia amekuwa mgonjwa kwa muda  na anahitaji sana msaada wetu wa kimaadili, kiakili na zaidi wa kifedha ili kumudu gharama za matibabu ambazo ni zaidi ya Sh milioni 1.5,” alisema Kajei Salim.

Kajei alifichua kuwa familia ya mwanamuziki huyo imepanga kuchangisha pesa ili kujaribu kukusanya kiasi kinachohitajika hospitalini.

Aliwataka mashabiki, marafiki, na wasanii wenzake kumsaidia mwanamuziki huyo ambaye ni mgonjwa katika tarehe waliyopanga kwa ajili ya kuchangisha pesa.

"Dick na familia yake wameandaa uchangishaji fedha utakaofanyika tarehe 26 Novemba 2022 katika makazi yake katika Kijiji cha Githuya saa nane jioni. Tafadhali tumuunge mkono gwiji wetu sasa kwa kuwa anatuhitaji sana," aliongeza.

Dick alikuja kujulikana hadharani mnamo 2021 baada ya wimbo wake 'Firirinda' kupamba vichwa vya habari kwenye mitandao ya kijamii baada ya mtangazaji wa redio anayefanya kazi katika kituo cha redio cha humu nchini, Jeff Kuria kuusambaza kwenye mitandao ya kijamii na kuchukua mtandao kwa dhoruba.

Firirinda ni wimbo wa kitamaduni unaoonyesha uchangamfu na furaha ya kuwakaribisha wageni na uliovuma kwa miezi kadhaa nchini Kenya haswa kwenye Twitter karibu miaka 35 baada ya kuachiliwa.