Eric Omondi ajibu baada ya kukosolewa kwa kurekodi mpenziwe baada ya kupoteza ujauzito

Omondi alisema kuwa aliwataka watu kuelewa uchungu ambao wanawake hupitia

Muhtasari

•Eric alijibu hatua ya wanamitando kumkemea alipopakia video hiyo na kuweka wazi kwamba hakuwa akitafuta kiki..

• Kwa kuwa ulikuwa ujauzito wa kwanza wa Lynne, walikosa kuelewa kilichokuwa kikiendelea.

Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Mchekeshaji Eric Omondi amevunja kimya baada ya kukosolewa kwa kuchapisha video ya mpenzi wake, Lynne baada ya kupoteza ujauzito.

Katika mahojiano yake na Mboya Vincent, alieleza kuwa mpenziwe alianza kulalamika kuhusu maumivu ya tumbo kabla ya ujauzito wake kuharibika.

"Nilipata taarifa hiyo baadaye kisha nikaelekea kumchukua Lynne nyumbani ili kumpeleka hospitali, ni kitu ambacho siwezi taka mtu yeyote apitie," alisema.

Kwa kuwa ulikuwa ujauzito wa kwanza wa Lynne, walikosa kuelewa kilichokuwa kikiendelea.

Eric alijibu hatua ya wanamitando kumkemea alipopakia video hiyo na kuweka wazi kwamba hakuwa akitafuta kiki.

Mchekeshaji huyo alisema kuwa hilo ni jambo kubwa  lisilo la kuchezewa  wala kutumiwa kutafuta kiki.

"Madaktari walikuwa wanatutarajia, nilipata ujumbe baada ya saa tano. Wakenya wanafaa kuwa wenye akili. Kuna mambo ambayo hatuwezi kutania. Mambo kama vurugu au ukatili, ubakaji na hata kumpoteza mtoto," alisema.

Eric alifichua kuwa Lynne alikuwa na maumivu ya tumbo kwa siku tatu ila wakati alipopoteza ujauzito wake alipitia maumivu kwa saa sita bila kuacha.

Alisema kuwa matukio kama hayo ni mambo ya kimaisha bali si mambo ya kuwaburudisha watu.

"Kwa mara nyingi huwa tunasikia watu wakisema wamejifungua, wamepoteza ujauzito wao au wamepata maumivu ya kujifungua. Huwa hatuelewi vyema. Hatukuwa tumejua jinsia ya mtoto wetu bado kwani ujuauzito huo ulikuwa mdogi bado," alisema.