Harmonize ajigamba kufanikiwa mbele ya Diamond na mameneja wa WCB

Amchana Diamond na kumuita Asake wa Tandale huku pia akimtukana meneja Sallam SK kama kipara.

Muhtasari

• Anazidi kutupa lawama kwa upande huo wa WCB Wasafi akiwachana kuwa sasa hivi si rahisi kumfanyia mtu fitina kimuziki ili kuizima nyota yake.

Harmonzie, Diamond Platnumz
Harmonzie, Diamond Platnumz
Image: Instagram

Jumatatu alasiri, msanii Kontawa aliachia ngoma yake remix ya ngoma Champion ambayo amemshirikisha msanii Harmonize.

Gumzo kubwa la ngoma hiyo ni kwenye vesi ya Harmonize ambaye ameamua kutupa vipondo kwa lebo ya WCB iliyomlea na kumtoa kimuziki.

Harmonize ambaye katika siku za hivi karibuni ameonekana kukumbatia falsafa ya ‘kufa gari kufa dereva’ aliendeleza mashambulizi yake dhidi ya Diamond Platnumz huku akimkejeli kwa madai ya kusemekana kuiba wimbo wa msanii Asake.

Kwenye vesi hiyo, msanii Harmonize anamkausha Diamond na kumtaja kuwa Asake wa Tandale huku pia akijipoga kifua kuwa ametoka nyuma na kufanikiwa zaidi kuliko mameneja wake akina Babu Tale na Mkubwa Fella.

“Nimetoboa mbele ya Mkubwa na Tale, kipara (Sallam SK) na Asake wa Tandale. Hizi sio zama za kale, muziki upo huru kama kambi ya kambale,” Harmonize anasikika akiimba kwa ukakamavu na unyama mwingi.

Anazidi kutupa lawama kwa upande huo wa WCB Wasafi akiwachana kuwa sasa hivi si rahisi kumfanyia mtu fitina kimuziki ili kuizima nyota yake kwani kila kitu kipo wazi kwenye majukwaa ya kidijitali. Kama mtu ni mpambanaji atatoka tu hata umkanyagie chini kivipi.

Msanii huyo katika katika wimbo wake wa My Way alimchoma Diamond kwa kisu chenye makali kuwili kwa kumsuta vikali kwamba alikuwa anamfanyia fitina ili asifanikiwe kimuziki kwa sababu alikuwa anaogopa Harmonize kumpita kimuziki na kuwa hicho ndicho kilikuwa chanzo cha bifu yake na yeye.