Lung'aho amsifia Matubia kwa uvaaji, awakosoa wanaosema hakuvaa vizuri

Mimi nilikuona kwa macho na ulikuwa unapendeza, wale wanaosema waliona kwa picha tu - Lung'aho alimwambia.

Muhtasari

• Matubia aliwataka wote waliokosoa uvaaji wake wakati mwingine kumwambia awape kazi ya kumchagulia nguo.

Wapenzi waigizaji Lungaho na Matubia
Wapenzi waigizaji Lungaho na Matubia
Image: YouTube screengrab

Wapenzi Jackie Matubia na Blessing Lung’aho kwa mara ya kwanza wamevunja ukimya kuhusu jinsi mashabiki walivyowatupia maneno ya kila rangi wakati walipakia picha zao baada ya kuhudhuria onyesho la kwanza la filamu ya Black Panther – Wakanda Forever.

Wawili hao walikuwa wanazungumza kupitia chaneli yao ya YouTube ambapo walisema wakenya wengi ambao ni mashabiki wao mitandaoni wana weledi wa kukejeli na kutoa komenti zenye kuchekesha kuhusu maisha na mienendo ya kimaisha ya watu.

Kulingana na mama huyo wa watoto wawili, walipokea mwaliko wa usiku wa manane, kwa hivyo waliona asubuhi iliyofuata ambayo ilikuwa ni taarifa fupi ya kupata mbunifu wa kufanya waonekane vizuri jinsi mashabiki wao walikuwa wanataka.

Alieleza kuwa alimpigia simu mbunifu mmoja na kumtaka amsaidie mavazi ya kuvaa kwenye hafla hiyo na kwamba kuna baadhi ya vitu alilazimika kuvalishwa akiwa amesimama karibu na mbunifu huyo. Hata hivyo, aliomba radhi kwa utani na kuahidi kufanya vizuri zaidi kwa tukio lijalo hata Blessing alieleza kuwa walithamini ukosoaji huo kwani ulitoka mahali pazuri na bila matusi.

“Mumetuingililia the Lung'ahos. Sijui mara nimesahau corset nyumbani, mara tulienda baby shower, watu wlikuwa na komenti za kuchekesha mpaka tukaanza kucheka. Nilijiona nimependeza, pengine sikukidhi matarajio ya watu, samahani. Tutafanya vizuri zaidi. Wakati ujao, tutafanya uchunguzi kwa ajili yenu nyote, mkuje mtupee anabuni zenu, tuwaulize mnataka tuvae nini,” Matubia alisema huku wakitabasamiana.

Blessing hata hivyo alimpongeza Jackie na kusema kwamba anaonekana mzuri sana ikilinganishwa na kile ambacho watu waliona kwenye mitandao ya kijamii.

"Unajua mimi niliona na macho, wale walikuona kwa picha ilipostiwa, sijui. Na ulionekana vizuri ajabu," aliongeza Blessing.