Zuchu alia kwikwi baada ya watu wachache kujitokeza katika shoo yake Marekani

Kulingana na taarifa ambazo hazijadhibitishwa, watu chini ya 50 pekee walijitokeza katika shoo hiyo.

Muhtasari

• Shoo yangu kule Houston haikuenda kama nilivyotarajia lakini namshukuru kila aliyejitokeza kwa ajili yangu - Zuchu.

Msanii Zuchu
Msanii Zuchu
Image: Instagram

Msanii wa kizazi kipya kutoka Tanznaia, Zuchu ni mtu mwenye hasira na uchungu baada ya shoo yake nchini Marekani kuvutia umati mdogo zaidi kulingana na vyanzo vya habari kutoka nchini humo.

Zuchu alianza ziara yake ya muziki nchini Marekani wiki jana na Jumamosi alikuwa anatumbuiza katika jimbo la Texas, Houston ambapo alipigwa na butwaa baada ya mashabiki wachache kujitokeza kwa ajili ya kumshabikia na kuhudhuria shoo yake.

Taarifa ambazo hazijadhitibishwa zinadai kuwa watu wasiozidi 50 walijitokeza kwa ajili ya kuhudhuria, jambo ambalo lilimpa mshangao mkubwa Zuchu na kupitia Instagram story yake alielezea mfadhaiko wake na kusema kwamba yote kwa yote anamuachia Mungu.

“Kama msanii, hakuna mtu anayeweza kukuandaa kwa nyakati kama hizi. Shoo yangu kule Houston haikuenda kama nilivyotarajia lakini namshukuru kila aliyejitokeza kwa ajili yangu. Nawapenda nyote,” Zuchu alisema.

Alidokeza kwamba mfadhaiko huo ulimpa machozi na uchungu ila akaahidi kuwa ni funzo ambalo amelipata na kuwa siku zijazo atazidi kutia bidi kimuziki.

Vie vile, alidokeza kwamba siku za hivi karibuni alipunguza kasi yake ya kufanya muziki mzuri na kuahidi kuwa atajirudi na kurekebisha kila kitu kabla ya pengine kuandaa ziara nyingine ughaibuni.

“Hii ya leo imenipa hasira ya kufanya zaidi. Hivi karibuni nilipoteza nguvu ya kufanya kazi kwa bidii, kibinadamu tu nilianza kujiuliza mbona nikachagua kazi kama hii lakini nyakati kama hizi zinanipa majibu kwamba wachache walioteuliwa hutolewa kama mfano ili ije kuwa rahisi kwa wengine,” msanii huyo aliandika ujumbe mrefu wenye mfadhaiko ndani yake.

Alitolea mfano wa bosi wake Diamond na kusema kuwa huenda hata yeye kabla kujizolea umati mkubwa aliyapitia naye akajipa Imani kuwa ipo siku atafika viwango kama hivyo.

Zuchu alisema kuwa amekubali kufeli katika shoo hiyo yake kwani ni moja ya njia nzuri za kumwelekeza katika mafanikio.