Zuchu awavisha koja la maua Nandy, Maua Sama na Rosa Ree

Zuchu alishinda tuzo ya Afrimma kweney kitengo cha Best Female East Africa.

Muhtasari

• Nawashukuru sana wanawake wote nyumbani na kila mwanamke anayeupambania muziki wa Afrika Mashariki

Zuchu awavulia kofia wasanii wa kike Tanzania
Zuchu awavulia kofia wasanii wa kike Tanzania
Image: Instagram

Kwa mara ya kwanza Zuchu ameonesha kutokuwa na chuki ya ushindani baina yake na wasanii wenzake wa kike kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na haswa nyumbani kwao Tanzania.

Hili lilidhihirika wazi baada ya kupokezwa tuzo ya AFRIMMA Jumamosi usiku huko Dallas Marekani ambapo katika hotuba yake aliwataja wanawake wanaopambania muziki wa Afrika Mashariki ili kukua kwa kasi na kupata picha ya utambulisho kote duniani.

“Ni miaka miwili tu nimekuwa kwenye gemu kama msanii chipukizi na leo hii nipo hapa nimeishikilia hii tuzo, nawashukuru sana wanawake wote nyumbani, Nandy, Maua Sama, Rosa Ree na kila mwanamke anayeupambania muziki wa Afrika Mashariki,” Zuchu alisema kwa hisia nyingi.

Pia aliwatambua mamake na bosi wake Diamond Platnumz kwa kuwataja kama mashujaa ambao siku zote watakuwa na nafasi ya kipekee kweney moyo wake kadri anavyozidi kupumua.

Zuchu kumtambua Nandy ilikuwa kama mshangao mkubwa kwa baadhi ya wadau wa muziki haswa baada ya wengi kudai kuwa huenda kulikuwepo na damu mbaya baina yao. Hi ni baada ya sauti kuvujishwa ikidaiwa kuwa ya Nandy akimkandia Zuchu kwa ubalozi wa kampuni ya vilevi nchini Tanzania miezi michache iliyopita.

Sauti inayodaiwa kuwa ya msanii Nandy akisikika akimueleza mtangazaji mmbea Mwijaku kumkandia chini Zuchu na kumchafua kwamba si eti alikataa dili lile bali dili lenyewe hakuitwa wala kulipata.

Sauti hiyo inayosemekana kuwa ya Nandy inazidi kutoa maelezo kwa Mwijaku na kumtaka asambaze uvumi kwamba Zuchu hakuitiwa mahojiano ya dili hiyo ya ubalozi wa kampuni ya vileo bali nandy alipewa moja kwa moja baada ya kukosekana mshindani kwenye Mahojiano ya kupata balozi wa matangazo ya biashara ya kampuni hiyo.