DJ Mo: Mtangazaji Anto Neosoul alinipa 'konekishen' ya mke wangu Size-8

Baadae, Mo alichangia kwa kiasi kikubwa kumbadilisha Size 8 kutoka kuimba miziki ya kidunia na kuanza kuimba injili

Muhtasari

• Anto ana ‘uchawi’ fulani. Ana uwezo wa kukutafutia mke kwa sababu alinifanyia hivyo hivyo. - DJ Mo.

DJ Mo adhibitisha Neosoul ndiye alimuunganisha na mkewe
DJ Mo adhibitisha Neosoul ndiye alimuunganisha na mkewe
Image: Instagram

Mcheza santuri wa muda mrefu DJ Mo amefunguka kuwa mtangazaji na mwanamuziki Anto Neosoul ndiye aliyempigia pasi ya kiuhakika ili kumpata mkewe Size 8.

Mo alifichua haya wakati mtangazaji huyo anayefanya katika kituo kimoja cha redio humu nchini alimpigia simu baada ya kubishana na mzalishaji wa kipindi chake aliyekataa kuamini kuwa Neosoul ndiye aliyewakutanisha Size 8 na mumewe DJ Mo.

Neosoul alikuwa ameambia produsa wake kuwa ni yeye aliyekuwa nyuma ya kujuana kwa DJ Mo na Size 8 kipindi hicho akiwa mwanamuziki wa miziki ya kidunia, lakini produsa alikataa kuamini jambo lililomfanya Neosoul kumtafuta kwa njia ya simu DJ Mo ili kudhibitisha.

Mo alidhibitisha kuwa wakati huo walikuwa sehemu na Neosoul na alipoona Size 8 akamtuma ili kuenda kumuita kwake na hivyo ndivyo hiyo bet iliiva.

“Inabidi uamini kuwa Anto ana ‘uchawi’ fulani. Ana uwezo wa kukutafutia mke kwa sababu alinifanyia hivyo hivyo. Nilimwambia aende kuniita yule bibi (akimaanisha Size 8), akafanya. Sasa angalia tulipo,” DJ Mo alisema kwa furaha na kumbukumbu.

Baada ya hapo, Mo alichangia kwa kiasi kikubwa kumbadilisha Size 8 kutoka kuimba miziki ya kidunia na kuanza kuimba injili ambapo mpaka sasa amejishindia tuzo kochokocho katika fani ya miziki ya injili.

Mwaka jana Size 8 alitawazwa kama mchungaji baada ya kumaliza kosi ya kosomea uchungaji na sasa anahubiri neno na pia kupitia nyimbo za kuutangaza ufalme wa Mungu.

DJ Mo na Size 8 ndio wanandoa mashuhuri ambao wamekuwa wakitumiwa kama kielelezo bora na watu wengi humu nchini tangu mwaka 2013 walipofunga ndoa yake katika ofisi ya mwanasheria.

Hivi majuzi katika mahojiano na mwanablogu Eve Mungai, DJ Mo alifichua kuwa hata kama hawajakaa kwenye ndoa zaidi ya miaka 10, watu wengi wanatafuta ushauri wa ndoa kwao ikiwemo watu wazima waliokubuhu kiumri hata kuwaliko na hilo linakuwa kama faraja kubwa sana kwao.

Wawili hao wanaendeleza mradi wa kujenga nyumba yao ya kifahari ambayo Mo alisema mapema mwaka kesho itakuwa inakamilika. Wamebarikiwa na watoto wawili.